• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 8:11 PM
Wakazi wa Muri Farm wapata hatimiliki za vipande vyao vya ardhi

Wakazi wa Muri Farm wapata hatimiliki za vipande vyao vya ardhi

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wapatao 400 wa Muri Farm, Kaunti ya Machakos, leo Jumanne wamepokea hatimiliki kupitia shirika la kilimo la Agricultural Finance Corporation (AFC).

Gavana wa Kaunti ya Machakos Dkt Alfred Mutua aliyekuwa mgeni wa heshima ameshuhudia hafla hiyo iliyohudhuriwa na wakazi wengi wa eneo hilo.

Mwenyekiti wa bodi ya AFC Bw Franklin Bett, na mkurugezi wake Bw Lucas Meso, wamewahimiza waliopokea vyeti vyao kuwa makini na wasijaribu kuuza kiholela vipande vyao vya ardhi.

“Hii ni njia moja ya serikali kuona ya kwamba kila mwananchi anaishi maisha ya kutamanika bila kuhangaika,” amesema Bw Bett.

Amewahimiza wakazi wa eneo hilo ambao bado hawajakamilisha malipo yao ya vipande vya ardhi wafanye hivyo mara moja ili washughulikiwe kama wengine.

Mwenyekiti wa bodi ya shirika la AFC Bw Franklin Bett (kushoto) akiwa na Gavana wa Kaunti ya Kiambu Dkt Alfred Mutua. Picha/ Lawrence Ongaro

Shule ya msingi ya Matema na ya upili ya Muri ni miongoni mwa asasi zilizopokea hatimiliki.

Gavana Mutua kwa upande wake amepongeza AFC kwa kufanya juhudi kuona ya kwamba maskwota wa Muri Farm wamepata haki yao ambayo ni kupokea hatimiliki.

“Sasa kila mmoja hapa atajisikia kama Mkenya halisi kwa sababu yuko kwake nyumbani, na hakuna yeyote atakayejaribu kumtatiza,” amesema Dkt Mutua.

Amemhimiza Rais Uhuru Kenyatta kuhakikisha pesa za mafuta ghafi ambayo yameanza kuuzwa zimelindwa kutoka kwa waporaji.

“Rais anastahili kuwa macho fedha hizo zisipitie kwa mikono ya waporaji ambao wamezoea kunyakua kila kitu kipitacho mbele yao,” amesema Dkt Mutua.

Amesema viongozi wanastahili kufanya kazi kwa pamoja kwa minajili ya kuboresha maisha ya wananchi.

Aidha, amewahimiza wakazi wa eneo hilo kukaribisha maafisa wa sensa kwa sababu itaisaidia serikali kupanga mambo yake ya baadaye.

Amewasifu viongozi waanzilishi wa siasa za nchi ambao waliweka misingi bora ya uongozi ambayo raia wanajivunia kwa sasa.

“Viongozi kama Hayati Mzee Jomo Kenyatta, marehemu Jaramogi Oginga Odinga, Daniel Moi, na Mwai Kibaki ni nguzo muhimu katika nchi hii na wanafaa kuheshimiwa,” amefafanua gavana huyo.

Amesema ifikapo mwaka wa 2022 yeye kama kiongozi mwenye ujuzi katika serikali ya hapo awali ya Mstaafu Kibaki, na kama gavana, atajiwasilisha mbele ya Wakenya kuwania kiti cha urais.

“Nitalazimika kuzunguka nchi yote ya Kenya ili nijitambulishe kwa wananchi nikitafuta uungwaji mkono. Ninajua ni kibarua kizito lakini kwa kumtegemea Mungu mambo yatakwenda sawa,” amesema Dkt Mutua.

Mkazi mmoja wa eneo hilo ambaye ni mfugaji Bw Pilipili Lekmarere, 60, anasema amefurahi baada ya kupata hatimiliki ya kipande cha ardhi huku akipongeza AFC kwa kuharakisha ombi lao.

Mwenyekiti wa bodi ya shule ya msingi ya Matema na ya upili ya Muri Bw David Nthama, amesema ni furaha kuu kwa shule hizo mbili kupata haki yao.

Bi Mary Njoki pia hakuficha furaha yake baada ya kupokea cheti chake.

“Ni zaidi ya miaka 15 tumekuwa tukipigania haki yetu lakini leo yote yametimia. Mungu ni mkubwa,” amesema Bi Njoki.

You can share this post!

Kiwanda cha maziwa cha Daima chafungwa kwa uchafuzi wa Mto...

TEKNOLOJIA: Kijana ajizatiti kutengeneza mtambo wa kuwasha...

adminleo