Wakazi wafunzwa mbinu mpya ya 'kumulika hongo'
PETER MBURU na MERCY KOSKEY
VIONGOZI wa usalama waliungana na maafisa wa Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC) kaunti ya Nakuru Jumatano kuongoza matembezi na uhamasishaji kwa umma ili waripoti visa vya ufisadi kupitia simu za mkononi.
Wakiongozwa na kamishna wa kaunti hiyo Joshua Nkanatha na kamanda wa polisi Hassan Barua, viongozi hao walishirikiana na shirika la ‘Mulika Hongo’ kuhamasisha umma kuhusu namna bora, mpya na salama ya kufanikisha vita dhidi ya ufisadi.
Kulingana na mratibu wa shirika hilo wa kitaifa Bi Grace Wanjohi, wananchi ndio nguzo muhimu katika kupigana na ufisadi nchini, endapo watakubali kuripoti visa hivyo wanapokumbana navyo, ama kukataa kutoa rushwa.
Walizindua mbinu ya kutumia ujumbe mfupi kwa simu ya rununu ama apu kwa simu za kisasa zenye mifumo ya Android kuripoti visa hivyo kwa haraka na kwa njia salama.
“Kupitia njia hii, zaidi ya macho milioni 40 yameweza kuona na kuripoti visa vyote vya ufisadi popote, wakati wowote na dhidi ya yeyote. Mafanikio yetu mkuu ni uwezo wa kuzuia ufisadi kwani waendeshaji wanaripotiwa kwa njia salama,” akasema Bi Wanjohi.
Kulingana na kamishna wa kaunti ya Nakuru Bw Joshua Nkanatha, ni jukumu la kila mtu kupigana na ufisadi na wote, anayetoa na anayepokea rushwa watakabiliwa kisheria, ila lawama haipaswi kuwaangukia wanaopokea pekee.
“Kamati ya usalama Nakuru ilifanya mikutano mingi na ikaamua kupigana na suala la ufisadi ana kwa ana na hafla hii itaandaliwa kila mwaka ili kufanikisha vita hivi.juhudi sasa ni kujumuisha wananchi katika vita dhidi ya ufisadi kwani ndio wanaoumia zaidi na visa vya ufisadi,” Bw Nkanatha akasema.
Naibu mkurugenzi wa EACC eneo la South Rift Bw Gilbert Lukhoba alisema kuwa Mulika Hongo ilikuwa mbinu muhimu ya kupigana na ufisadi, akirai wakenya kushirikiana na mashirika yote yanayofanikisha vita hivyo.
“Viongozi wa dini, wazazi, walimu na wote wanafaa kueneza maadili mema ili taifa lijivunie mazao mema siku za usoni,” akasema Bw Lukhoba.