Afueni kwa wakazi mradi wa barabara kupunguza ujambazi
NA KALUME KAZUNGU
MRADI wa ujenzi wa barabara ya kilomita 15 unaoendelezwa kwenye mji wa Mokowe, Kaunti ya Lamu umesaidia pakubwa kupunguza visa vya utovu wa usalama na wizi uliokuwa ukishuhudiwa eneo hilo.
Barabara hiyo ambayo tayari imekamilika kwa zaidi ya asilimia 10 inajengwa kupitia Halmashauri ya Ujenzi na Ustawi wa barabara za maeneo ya miji (KURA).
Jumla ya Sh 1.1 bilioni zimetengwa kwa minajili ya ujenzi wa barabara hiyo inayolenga kurahisisha usafiri wa wakazi hasa wakati wanapotafuta huduma za serikali kwenye makao makuu ya kaunti yaliyoko mjini Mokowe.
Wakizungumza na wanahabari mjini Mokowe Alhamisi, wakazi walikiri kuwa kuajiriwa kwa mamia ya vijana kwenye mradi huo ni changizo kubwa iliyopelekea kupungua au kumalizwa kabisa kwa visa vya wizi na ujambazi uliokuwa ukiendelea mitaani.
Mwakilishi wa vijana eneo hilo, Bw Issak Yunus, alisema kipindi cha miezi kumi tangu kuanzishwa kwa mradi huo wa barabara eneo lao kimeshuhudia utulivu wa hali ya juu.
Vibarua
Alisema idadi kubwa ya vijana waliokuwa wakirandaranda mitaani bila ajira kwa sasa wamejipatia vibarua kwenye ujenzi wa barabara.
“Tunashukuru sana shirika la KURA kwa kutuletea mradi wa barabara eneo letu. Usalama umeimarika kwani vijana ambao walikuwa wakiendeleza wizi na ujambazi barabarani wamejipoatia kazi katika ujenzi wa barabara,” akasema Bw Yunus.
Naye Bi Marita Kariuki, alisema mbali na vijana kupata kazi, biashara pia imenoga mjini Mokowe hasa tangu barabara za mji huo zilipoanza kujengwa.
Alisema idadi ya wanabiashara wanaotekeleza shughuli mjini humo pia imeongezeka katika siku za hibvi karibuni.
Wateja wengi
“Baadhi ya wanabiashara tayari wameanza kuhamisha makazi yao kutoka kisiwa cha Lamu hadi Mokowe. Wateja wamekuwa wengi ilhali wafanyabiashara wanaofungua shughuli zao mjini Mokowe pia inaongezeka kila kuchao,” akasema Bi Kariuki.
Akizungumza wakati wa ziara yake eneo la Mokowe jana, Afisa Msimamizi wa KURA, Bw Mohamed Abdurashid, alisema lengo lao ni kuhakikisha barabara hiyo inakamilika kufikia Novemba, 2019.
Bw Abdulrashid alisema jumla ya kilomita 1.7 ya barabara hiyo tayari imekamilika kujengwa.
“Barabara yenyewe inajengwa kwa muundo wa kisasa. Tunalenga kufikia Novemba, 2019 tuwe tumekamilisha ujenzi wa barabara hii. Ikumbukwe kuwa kura pia inatekeleza miradi sawia na huu katika kaunti 14 za hapa nchini,” akasema Bw Abdulrashid.