Habari Mseto

Wakazi wakataa mradi wa serikali wa nyumba nafuu

Na FRIDAH OKACHI April 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WAKAZI na wamiliki wa nyumba katika mtaa wa Korogocho wamepinga ujenzi wa nyumba za bei nafuu katika mkutano wa umma uliokuwa umeandaliwa na maafisa wa Serikali ya Kenya Kwanza.

Wakazi hao wanadai kuwa kamati ya kuboresha mtaa, wazee wa nyumba kumi pamoja na viongozi wa serikali ni wafisadi na wanawashinikiza wakubali mradi huo.

Kulingana na Bi Elizabeth Wangui anayemiliki nyumba 40, alisema walielezwa na maafisa hao kuwa serikali inapania kujenga nyumba za bei nafuu katika ardhi ambayo wameishi kwa miaka mingi na hawana mahali mbadala pa kuhamia.

“Hii ni ploti yangu ambayo nimemiliki kwa zaidi ya miaka 30 baada ya kuachiwa na mzazi. Hii ndio sehemu ambayo natumia kupata riziki yangu na hao maafisa hawasemi watatulipa fidia,” alisem Bi Wangui.

Alisema kuwa maafisa hao hawajatoa hakikisho kuwa baada ya kuondolewa kutoka sehemu hiyo watarejea kumiliki nyumba hizo.