Wakazi walia Kenya Power iliwabomolea nyumba 500 kinyume cha sheria
Na PETER MBURU
WABUNGE wa Kamati ya Kawi Ijumaa watazuru eneo la Chokaa, Embakasi Mashariki, Kaunti ya Nairobi kushuhudia jinsi kampuni ya Kenya Power iliwabomolea wakazi takriban nyumba 500, kwa madai kuwa walikuwa wamejenga katika ardhi yake.
Hii ni baada ya wawakilishi wa wakazi hao, wakiongozwa na mbunge wao Babu Owino kufika mbele ya kamati hiyo Jumanne, ambapo waliieleza kuwa kampuni hiyo iliwabomolea nyumba hizo na kuwaacha bila makao, licha ya kuwa iliwaruhusu kujenga.
Wakazi hao walisema kuwa licha ya kuwaambia mahali walipokuwa wakijenga hapakuwa hatari, maafisa wa Kenya Power waliwawekea stima, ambayo wamekuwa wakilipia, tangu 2009.
Nyumba hizo zilibomolewa mnamo Machi 10, wakazi wakidai kuwa wengi wao walichukua mikopo kununua ploti hizo na kujenga, na kuwa wameathirika sana.
“Kutokana na ubomozi huo watu wawili walifariki. Mmoja alijinyonga baada ya nyumba yake kubomolewa, naye mwingine akashtuka na kuanguka, kisha akafa- alipoona nyumba yake ikibomolewa,” akasema Bw Owino.
Wakazi walisema walikuwa wamekutana na maafisa wa kampuni hiyo mara kadhaa na kuhakikishiwa kuwa hakukuwa na tatizo, lakini wakashtukia wamebomolewa nyumba zao.