Wakazi wamsifu Naibu Gavana kuchukua usukani baada ya Obado kukamatwa
Na VIVERE NANDIEMO
JAMII ya Wakuria katika Kaunti ya Migori, imefurahishwa na jinsi Naibu Gavana Nelson Mwita Mahanga anavyoshika usukani kufuatiaa kukamatwa kwa Gavana Okoth Obado.
Hapo Jumanne, wakazi wa eneo la Kuria lililo katika kaunti hiyo, walijazana katika afisi za serikali ya kaunti kukutana na Bw Mahanga.
“Tunasimama imara na Gavana Obado na tunamtakia mema. Tulienda kumwona mtoto wetu na kumtakia mema anaposimamia shughuli za kaunti wakati gavana hayuko. Katiba inasema naibu gavana anastahili kushikilia usukani gavana anapoondoka,” akasema mmoja wa wakazi wa eneo la Ntimaru.
Wakati Bw Obado alipokuwa mahakamani Jumatatu, Bw Mahanga alisimamia mkutano na wawakilishi kutoka Benki ya Dunia, ambayo inafadhili miradi kadhaa ya kilimo katika kaunti hiyo.
Wakazi wengine wa Kuria waliandika kwenye mitandao ya kijamii kueleza furaha yao kuhusu uwezekano wa kuwa na gavana Mkuria katika Kaunti ya Migori.
Lakini furaha yao haikupokewa vyema na wafuasi wa Bw Obado ambao walisema si utu kusherehekea masaibu ya gavana wao.
“Inasikitisha kuwa watu tayari wanazungumza kuhusu gavana mpya wakati kesi inayomkabili gavana wetu haijaamuliwa na mahakama. Bado tunasisitiza kuwa gavana atapatikana hana hatia na tutafurahi kumkaribisha nyumbani,” akasema mmoja wa wafuasi wa Bw Obado.
Hali hii imeibua upya mizozano ya kisiasa kati ya jamii ya Waluo ambao ndio wengi Migori, na wenzao Wakuria walio wachache.
Jamii hizo mbili zimekuwa haziaminiani katika siasa. Kwa upande mmoja, Wakuria wamekuwa wakiegemea Chama cha Jubilee huku Waluo wakiwa wafuasi sugu wa upinzani.