Wakazi watahadharishwa kuhusu mafuriko
Na WAANDISHI WETU
MVULANA alikufa maji Jumanne kufuatia mvua kubwa inayoendelea kunyesha maeneo mengi ya Bonde la Ufa na kusababisha maafa.
Tahadhari kuu imetolewa kwa wakazi katika maeneo yenye hatari ya kukumbwa na mafuriko na mmomonyoko wa ardhi hususan Kaunti ya Baringo.
Uchunguzi wa Taifa Leo ulipata kuwa viwango vya maji katika Ziwa Baringo vinaongezeka kwa haraka mno, na kuweka hatarini vijiji vinavyozingira ziwa hilo.
Iiliripotiwa kuwa tineja aliyetumbukia majini alikuwa akijaribu kuvuka mto wa msimu kwenye soko la Eldoret |Magharibi, Kaunti ya Uasin Gishu.
Wazazi wa marehemu walisema kuwa alizama saa za alasiri akitoka dukani. Mwili huo uliondolewa majini Jumatano alasiri.
Mzee wa kijiji eneo hilo, Bw Jonathan Dungo aliambia wanahabari kuwa juhudi za kuondoa mwili huo mtoni zilikabiliwa na wakati mgumu kutokana na mafuriko yanayosababishwa na mvua kubwa inayonyesha sehemu hiyo.
Kifo hicho kilithibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Turbo, Bw Zachariah Bittok.
“Tunachukua kisa hicho kama ajali ya kawaida. Wakati wa msimu huu mito hufurika. Wananchi wanafaa kuwa waangalifu zaidi na kuepuka mito ambayo hufurika,” Bw Bittok alisema.
Wakati huo huo, wasafiri walikwama mjini Eldoret Jumanne usiku baada ya barabara nyingi kushindwa kupitika.
Shughuli kwenye barabara kuu ya Eldoret-Nakuru zilikatizwa kwa saa kadha baada ya sehemu ya barabara hiyo kufurika, na kusababisha msongamano mkubwa wa magari.
Wahudumu wa bodaboda walipata donge nono kwa kuwatoza wapita njia kati ya Sh20 na Sh50 kuvuka barabara hiyo ambayo kwa kawaida huwa na shughuli chungu nzima.
Kwenye barabara ya Ronald Ngala mjini Eldoret maduka yalijaa maji kufuatia mafuriko.
Wakazi wa mji huo walihimiza wahandisi wa serikali ya kaunti kuzibua mitaro yote ya kuondoa maji taka ili kuondoa maji ya mafuriko mjini humo.
Hayo yakijiri, wataalamu wa jiolojia wametoa tahadhari kwa wakazi katika maeneo yenye kukumbwa na maporomoko ya ardhi Bonde la Ufa.
Wataalamu hao walitaja hususan miji ya Kabasis, Kasisit na Timboiywo katika Kaunti ya Baringo.
Katika vijiji vya Kokwo, Ng’ambo, Sintaan, Loropil, Salabani, Leswo, Longewan, Ildepe-Osinya, Eldume na Ilng’arua vinavyozingira Ziwa Baringo, wakazi wamehimizwa kuwa macho zaidi kufuatilia ongezeko la viwango vya maji ziwani.
Jumatatu, idara ya utabiri wa hali ya hewa ilitangaza kuwa mvua iliyoanza kunyesha wiki iliyopita, itaendelea kushuhudiwa maeneo mengi nchini. Pia ilitahadharisha kuwa upande wa Mashariki ungeshuhudia upepo mkali.
Ilisema mvua itanyesha maeneo ya Ziwa Victoria, nyanda za juu za Bonde la Ufa kwa muda wa siku nne.
Maeneo ambayo pia yanatarajiwa kupokea mvua ni Siaya, Kisumu, Homa Bay, Migori, Kisii, Nyamira, Trans Nzoia, Baringo, Uasin Gishu miongoni mwa mengine.
Mkurugenzi Mkuu wa idara hiyo, Bi Stella Arua, alieleza hayo alipotangaza kuhusu utabiri huo wa hali ya hewa inayotarajiwa nchini.