Habari Mseto

Wakenya waishangaa CBK kusambaza noti za zamani za Sh1,000

July 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na PAUL WAFULA

BENKI Kuu (CBK) imekosolewa kwa kuendelea kusambaza noti za zamani za Sh1,000 huku makataa ya kurudisha noti hizo benki ukiendelea kuyoyoma.

Wakuu walioomba wasitajwe gazetini, walisema wanashangaa kwa nini noti za Sh1,000 zinazostahili kuondolewa sokoni zingali zinasambazwa badala ya zile mpya.

Uchunguzi wetu katika mitambo ya ATM katikati mwa jiji la Nairobi, ulionyesha kuwa kuna noti mpya za muundo wa zamani ambazo zimetolewa hivi karibuni.

Maeneo mbalimbali yenye mashine ya uegeshaji magari pia hayakubali noti mpya, wiki tano baada ya serikali kutangaza kuwa noti hizo ndizo zitakuwa zikitumika.

Mameneja kadha waliahidi kuwa mitambo ya ATM itaundwa upya ili ziweze kutoa noti mpya.

Mnamo Juni 1 mwaka huu Gavana wa CBK, Patrick Njoroge alisema kuwa mpango wa kuondolewa noti hizo za zamani ni mojawapo ya mbinu za kuhakikisha wanaoficha pesa hizo manyumbani wanazirejesha.

Aliongeza kuwa mpango huo ni njia mojawapo ya kupambana na ufisadi na uhalifu wa kiuchumi.

“Kuanzia Oktoba 1, noti zote za zamani za thamani ya Sh1,000 ambazo hazitakuwa zimerejeshwa zitakosa thamani,” Dkt Njoroge akasema.

Hatua hiyo ilikosolewa kama isiyo na nia ya kukabili wafisadi kutokana na muda mrefu wa miezi minne uliotolewa.

Wakosoaji walisema walioficha pesa watakuwa nma muda wa kuzitumia.