Habari Mseto

Wakenya walio China wasema pesa si muhimu

February 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

MARY WANGARI na PHYLIS MUSASIA

Zaidi ya Wakenya 3,000 waliokwama katika mkoa wa Wuhan, nchini China kutokana na mkurupuko wa Homa ya China, watalazimika kusubiri kwa muda zaidi huku ripoti mpya zikiibuka kuhusu masaibu wanayokabiliana nayo.

Licha ya msemaji wa serikali Kanali Cyrus Oguna kutangaza jana kuwa serikali imetoa Sh1.3 milioni kuwasaidia wanafunzi 91 waliokwama Wuhan, imebainika kuwa huenda msaada huo usiwafae chochote.

Wakizungumza na Taifa Leo jana kupitia WhatsApp, wanafunzi hao walifichua kuwa wanakabiliwa na wakati mgumu kwenda madukani au katika vituo vinginevyo vinavyouza bidhaa za kimsingi kufuatia ulinzi mkali uliomo mkoani Wuhan, ambao ni kitovu cha mkurupuko wa virusi hivyo hatari.

Kulingana na wanafunzi hao waliojawa hofu, japo wanaishukuru serikali kwa kuwapa msaada wa kifedha, shaka lao ni kurejeshwa nchini ili waweze kutulia kimawazo.

“Taharuki imetanda huku japo serikali inasema itatupatia pesa za matumizi, sidhani zitatusaidia kwa vyovyote. Hatuwezi kununua chakula ama kitu kingine chochote madukani au mitandaoni kutokana na msako uliopo,” alisema mwanafunzi Mkenya wa chuo kikuu mjini Wuhan katika mahojiano jana.

Mwanafunzi huyo alisema amefungiwa katika bewa la taasisi hiyo kwa majuma matano pamoja na wengine huku ikiwa vigumu kupata bidhaa za kimsingi ikiwemo chakula na maji.

Akihutubia vyombo vya habari jijini Nairobi jana, Msemaji wa Serikali Kanali Cyrus Oguna alisema serikali imetoa Sh1.3 milioni kwa lengo la kutoa msaada kwa wanafunzi 91 na wanasarakasi tisa, wakiwemo Wakenya wawili ambao ni wajawazito.

Bw Oguna alisema serikali inashirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Wizara ya Kigeni, Shirika la Msalaba Mwekundu pamoja na Ubalozi wa China ili kutoa msaada wa bidhaa muhimu kwa Wakenya hao.

“Serikali imetoa Sh1.3 milioni pamoja na ufadhili wa Sh500,000 kutoka kwa Ubalozi wa China nchini ili kutoa msaada wa vyakula, matibabu na vifaa vingine muhimu kwa watoto wetu walio China. Wakenya wawili ambao ni wajawazito pia wameweza kupokea msaada muhimu wa vyakula na matibabu kupitia Ubalozi wa China,” alisema.

Msemaji huyo pia alifafanua kwamba serikali kwa sasa haitaweza kuwaondoa Wakenya China kutokana na hatari ya kuambukizwa ugonjwa huo hatari huku akisistiza kwamba hakuna Mkenya ambaye ameambukizwa kufikia sasa.

“Kuna makundi mawili ya Wakenya walio China; wafanyabiashara na watu wengineo ambao ni 3,000. Pia kuna wanafunzi na wanasarakasi wanaoishi katika maeneo mbalimbali mkoani Wuhan na wote wako salama popote walipo. Mkoa wa Wuhan ndio kituo kikuu cha elimu China ndiposa kuna idadi kubwa ya wanafunzi.

“Kuna hatari zaidi ya wao kupata virusi vya Homa ya China vinavyoambikizwa kupitia hewa ikiwa watasafiri ili kukusanyika katika eneo moja kwa lengo la kurejeshwa nchini. Kwa sasa ni bora wakae walipo huku tukiendelea kutathmini hali hasa wakati huu kiwango cha maambukizi ya COVID-19 kinapozidi kushuka China,” alieleza.

Aidha, serikali imeweka mikakati thabiti ikiwemo kuimarisha usalama katika vituo vya kuingia nchini, katika Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA), bandari na kutoa mafunzo kwa maafisa wa afya katika juhudi za kuzuia mkurupuko huo nchini.

“Tuna vituo 34 vya kuingilia nchini na vyote tumeimarisha ukaguzi. Kuna jumla ya maafisa 150 JKIA katika zamu tofauti. Maafisa wa afya wote wamepewa mafunzo muhimu huku vifaa 5000 vya kujikinga vikinunuliwa,” alisema. Kulingana na takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), mkurupuko wa Homa ya China kwa sasa umesababisha vifo vya watu 1,870 huku visa 73,332 vikithibitishwa kote duniani.