Wakenya wapewe fursa wajisomee ripoti ya BBI – Mbunge
Na TITUS OMINDE
MBUNGE Mwanamke wa kaunti ya Vihiga Bi Beatrice Adagala anataka wanasiasa wasilazimishe Wakenya kuunga mkono ripoti ya jopo la maridhiano (BBI).
Bi Adagala amesema Wakenya wa mashinani wanastahili kupewa muda wa kutosha kusoma ripoti ya BBI ili kufanya uamuzi sahihi bila kudanganywa na wanasiasa walio na masilahi ya ubinafsi.
Kiongozi huyo alisema kuwa viongozi wa mashinani wanapaswa kupewa kipaumbele kutoa elimu ya raia kuhusu BBI kwa lugha ambayo watu walio chini wanaelewa vizuri.
‘Hatupaswi kuajiri wageni kufundisha watu wetu juu ya BBI hii ni haki yetu ya baadaye na lazima iachwe kwa wenyeji kuukubali kupitia mchakato mzuri wa elimu ya raia katika ngazi ya chini ambapo Wakenya wote wanahusika,’ alisema Bi Adagala.
Akihutubu katika eneo la Emuhaya kaunti ya Vihiga Bi Adagala alisema ataunga mkno BBI Kwa kuzingatia uwezeshaji wa wanawake na vijana, kupambana na umasikini miongoni mwa maswala mengine ambayo yanaathiri mwananchi wa kawaida.
Msimao wake uliungwa mkono na mwenzake wa Uasin Gishu Gladys Boss Shollei ambaye alisema kwamba anaunga mkono BBI baada ya kubaini kuwa inasaidia Wakenya wa kawaida.
Bi Shollei ambaye awali alikuwa akipinga BBI alisema baada ya kusoma ripoti ya hiyo amegundua kuwa ni nzuri kwa Wakenya hivyo basi anaiunga mkono kwa manufaa ya Wakenya wote.
‘Hapo awali nilikuwa nikipinga BBI lakini sasa nimeshasoma waraka huo na nimebaini kuwa ina mustakabali mzuri kwa ustawi wa Wakenya wote haswa kwenye maswala ya uundaji wa ajira kwa vijana wetu, utoaji wa elimu, utawala bora kupambana na rushwa miongoni mw amaswala mengine,’alisema Bi Shollei.
Alitaka serikali iharakishe na kuitekeleza bila kuingiza siasa za mgawanyiko ndani yake.