Wakenya wengi walalamikia huduma mbovu na bei ghali ya Kenya Power
Na BARNABAS BII
KAMPUNI ya usambazaji umeme ya Kenya Power ina idadi kubwa zaidi ya malalamishi yanayowasilishwa kwa idara ya serikali ya kupokea malalamishi ya umma ikilinganishwa na mashirika mengine ya serikali, kwa mujibu wa ripoti.
Ripoti ya Tume ya Utendaji wa Haki (CAJ) inaonyesha kulikuwa na malalamishi 22,000 kwa miezi sita katika kipindi cha fedha cha 2017/2018 kutoka kwa wateja kuhusu jinsi kampuni hiyo inavyotatua matatizo yanayoripotiwa kwake.
“Kampuni hiyo ya umeme inatarajiwa kutoa huduma za hali ya juu kwa wateja kwa kusambaza umeme bila matatizo,” ikasema ripoti iliyoandikwa na afisa mkuu katika idara hiyo, Bw Bob Munoko.
Miongoni mwa malalamishi ni kuhusu kuunganishiwa umeme ambapo wateja walilalamikia jinsi kampuni hiyo inavyochelewa kutekeleza majukumu yake baada ya kupokezwa stakabadhi zinazohitajika.
Mengine ni kuhusu ada kubwa za umeme kupita kiasi ambapo wateja walisema huwa wanahitajika kulipa kiasi kikubwa kuliko kiwango cha umeme wanachotumia.
Kulingana na ripoti hiyo, malalamishi dhidi ya Idara ya Polisi wa Kitaifa zilikuwa asilimia 12.2 ya jumla ya zilizopokewa, huku Wizara ya Ardhi ikiwa na asilimia 8.7 ya malalamishi.
Wizara ya Usalama wa Ndani ilikuwa na malalamishi asilimia 8.6, Mahakama asilimia 7.9, Wizara ya Elimu asilimia 3.1 na Wizara ya Afya ikawa na kiasi kidogo zaidi cha malalamishi kwa asilimia 1.3.
Malalamishi mengi yalihusu usimamizi mbaya, kutohudumiwa kwa njia ya haki, kucheleweshwa kwa huduma miongoni mwa mengine.
“Kumekuwa na ongezeko la malalamishi yanayopokewa. Hii ni ishara kuwa kuna udhaifu katika mifumo ya uongozi wa mashirika ya umma, sera, mitindo ya kutoa huduma na uwezo wa mashirika hayo kutoa huduma bora kwa wananchi,” ikasema ripoti hiyo.
Ilipendekezwa mashirika hayo yaweke mikakati maalumu ya kuboresha utoaji huduma ili kukabiliana na changamoto zilizopo.
Meneja wa Mawasiliano katika idara ya kupokea malalamishi ya umma, Bw Sammy Cheboi, aliomba wananchi wawe wakiripoti maafisa wanaokosa kuwahudumia vyema ili hatua zichukuliwe dhidi yao.
Mashirika mengine ambayo yalikuwa na malalamishi mengi kutoka kwa umma ni Hazina ya Kuimarisha Uwekezaji wa Vijana (YEDF), Shirika la Nyama la Kenya (KMC) na Mamlaka ya Utengenezaji Bidhaa za kuuzwa nje ya nchi (EPZA).