Habari Mseto

Wakenya wengine 20 watimuliwa Amerika

April 1st, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANDISHI WETU

WAKENYA 20 ni miongoni mwa watu 100 waliofurushwa Marekani kutokana na swala tata la wahamiaji haramu huku wengine wakiwa ni raia kutoka mataifa jirani ya Somali na Sudan Kusini.

Polisi na maafisa wa idara ya uhamiaji uwanjani JKIA walisema ndege hiyo ya Omni International Airline ambayo ni ya kibinafsi ilibeba watu 114 na ilitua uwanjani humo Ijumaa asubuhi.

Wakenya hao baadaye waliruhusiwa kuenda nyumbani huku zaidi ya wasomali 60 na raia 24 kutoka Sudan Kusini waliobaki kwenye ndege hiyo wakisafirishwa hadi miji ya Mogadishu na Juba mtawalia.

Wahamiaji hao ndio mkumbo wa mwisho wa wahamiaji haramu wanaorudishwa hapa nchini kwa muda wa miaka miwili ambayo Rais wa Marekani Donald Triump amekuwa uongozini.

Zaidi ya wakenya 100 walihamishwa kutoka taifa hilo mwaka 2017 ambayo ilikuwa idadi kubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Mwaka wa 2016 wakenya 63 walirejeshwa kutoka taifa la Marekani. Mwaka jana idadi hiyo iliongezeka hadi 103.

Kulingana na maafisa wa uhamiaji, Marekani waliwatimua raia 2,134 kutoka mataifa yanayopatikana chini ya jangwa la Sahara kufikia Septemba 30 mwaka 2017.

Idadi hiyo ilikuwa mara mbili ya raia 920 waliofukuzwa kutoka taifa hilo mwaka 2016. Jumla ya raia 521 wenye asili ya kisomali walirejeshwa makwao mwaka jana ikilinganishwa na 198 mwaka 2016.

Ripoti kutoka idara ya uhamiaji ya Marekani inaonyesha kwamba raia 226,119 walikuwa nchini humo bila kufuata kanuni za uhamiaji na walirudishwa katika mataifa yao mwaka 2017.

Mwaka 2016 ambapo Rais Trump aliingia uongozini idadi hiyo ilikuwa 240,225 hii ikiwa ni ongezeko la watu 13,106.

Ripoti hiyo inaonyesha Marekani inazidi kuongeza juhudi zake katika kuwatimua raia ambao wanaishi nchini humo kinyume cha sheria. Wengi wa watu hao kwa sasa wanakamatwa na maafisa kutoka idara ya uhamiaji.

Wengi wa wanaorejeshwa haswa kutoka Bara la Afrika, wanasemekana wameishi Marekani zaidi ya muda unaotakikana kulingana na kipindi kilichoandikwa kwenye visa zao za kuishi nchini humo.

Hata hivyo, kesi nyingi zilizowasilishwa na wahamiaji katika mahakama za Marekani zinachangia kujikokota kwa mchakato wa kuwarejesha wengi wao.