• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 7:53 PM
Wakili aliyekatwa mikono katika mzozo wa mapenzi afariki

Wakili aliyekatwa mikono katika mzozo wa mapenzi afariki

PIUS MAUNDU na BENSON MATHEKA

WAKILI aliyedaiwa kukatwa mikono na afisa wa kike wa polisi mjini Wote, Kaunti ya Makueni wiki moja iliyopita, alifariki Jumapili katika hospitali kuu ya Kenyatta, Nairobi, alikokuwa amepelekwa kutibiwa majeraha aliyopata.

Wakili Onesmus Masaku alilazwa katika hospitali hiyo akiwa na majeraha mabaya baada ya kushambuliwa na Konstebo Nancy Njeri wa kituo cha polisi cha Makueni.

Polisi walikuwa wamepanga kumfungulia mashtaka ya kujaribu kuua lakini kufuatia kifo cha wakili huyo huenda akashtakiwa kwa mauaji.

Mwenyekiti wa tawi la Kusini mashariki la chama cha wanasheria nchini (LSK), Bw Mutisya Mutia aliambia wanahabari kwamba wakili huyo alifariki Jumapili.

“Ni huzuni sana kwa sababu tumempoteza wakili katika kisa cha kusikitisha. Tutafuatilia kesi hii kuhakikisha uchunguzi umefanywa vyema na kuona haki imetendeka,” alisema.

Inadaiwa kwamba wawili hao walikuwa wapenzi na wapelelezi wamekuwa wakifanya uchunguzi kwa lengo la kubaini ikiwa afisa huyo alitaka kulipiza kisasi baada ya uhusiano wao kuvunjika.

Mshukiwa atarudishwa kortini Ijumaa baada ya siku 14 ambazo polisi walipatiwa na Mahakama ya Machakos kumzuilia ili wafanye uchunguzi kukamilika.

Wakili huyo alitokwa na damu kwa wingi kufuatia majeraha mabaya aliyopata kwa kukatwa mikono kwa upanga.

Bi Njeri alidai kwamba wakili huyo alimwalika katika nyumba yake kumtambulisha kwa mpenzi wake mpya lakini akamlazimisha wafanye mapenzi.

Ripoti ya polisi kuhusu tukio hilo ilisema kwamba alichukua upanga na kumkata mikono ili kujinusuru kabla ya kutoroka. Hata hivyo LSK ilipuuza madai hayo na kuwalaumu polisi kwa kuficha ukweli.

Chama hicho kilisema wawili hao walikuwa wapenzi na kwamba afisa huyo alikasirika baada ya wakili huyo kukataa kumuoa.

Ni baada ya LSK kulalamika ambapo polisi walimkamata mshukiwa na kusema kwamba wangemfungulia mashtaka ya kujaribu kumuua wakili huyo.

Afisa huyo alipelekwa Mahakama ya Machakos polisi wakisema maisha yake yalikuwa hatarini kaunti ya Makueni kwa vile umma ulitaka kumshambulia.

Anazuiliwa katika kituo cha polisi kaunti ya Makueni.

You can share this post!

Wataka wafidiwe Sh10,000 kwa kila kondoo aliyeuawa na gari

Joto la siasa linafukuza wawekezaji – Atwoli