Habari Mseto

Wakili kutoka Uingereza aruhusiwa kuongoza mashtaka dhidi ya Mwilu

January 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

MAJAJI watano wa mahakama kuu Alhamisi walimruhusu wakili kutoka Uingereza Profesa Khawar Qureshi kuongoza kesi ya ufisadi dhidi ya Naibu wa Jaji Mkuu (DCJ) Philomena Mwilu.

Uteuzi wa Prof Qureshi kuwa kiongozi wa mashtaka maalum ni ushindi mkubwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji.

Uteuzi wa Prof Qureshi ulikuwa umekumbana na vizingiti na viziki vingi vya kisheria akidaiwa hajahitimu kuhudumu kuwa wakili kwa mujibu wa Sheria nambari 11 ya Sheria za Chama chama mawakili nchini (LSK).

Sasa Prof Qureshi ataanza kushiriki katika kesi hiyo dhidi ya Jaji Mwilu kwa kupinga walalamishi wengine  ambao ni Fida na wanaharakati.

Majaji watano waliomkubali wakili kutoka Uingereza Prof Khawar Qureshi kuongoza kesi ya Naibu wa Jaji Mkuu Philomena Mwilu. Picha/ Richard Munguti

Pia atatetea DPP katika kesi  ya kuomba mashtaka aliyofunguliwa Jaji Mwilu yatupiliwe mbali kwa vile hakutenda uhalifu kukopa pesa kwa benki iliyofungwa ya Imperial.

Jaji Mwilu anasema suala hilo la mkopo ni la kibiashara na “ hakuba makosa aliyofanya kuomba mkopo kwa benki.”

Mawakili James Orengo , Okong’o Omogen , Aulo Soweto, Daniel Maanzo, Dkt John Khaminwa na mawakili wengine zaidi ya 30 walipinga uteuzi wa Prof Qureshi wakisema ni  “fedheha kwa taaluma ya uwakili nchini.”

Walisema sheria za usakaji huduma za wakili maalum hazikufuatwa na kushirikishwa kwa umma kabla ya kumtambua Prof Qureshi kuongoza kesi dhidi ya Jaji Mwilu.

Naibu wa DPP Dorcus Oduor (anayesimama). Picha/ Richard Munguti

Mawakili hao walisema uteuzi wake mgeni huyo ulikaidi Vifungu nambari 10 na 157 za katiba na pia sheria nambari 85 inayoruhusu DPP kumteua wakili maalum kutekeleza majukumu yake.

“Tumehoji ushahidi wote uliowasilishwa na DCJ Mwilu kupitia kwa mawakili wake na kufikia uamuzi hakuna sheria ilikiukwa katika kumteua Prof Qureshi kuwa kiongozi wa mashtaka maalum,” walisema majaji hao watano.

Katika uamuzi wao , majaji hao walitupilia mbali ombi la Jaji Mwilu la kupinga Prof Qureshi akiongoza kesi dhidi yake.

Na wakati huo huo Majaji Hellen Omondi, Francis Tuiyot , Mumbi Ngugi , William Musyoka na Enoch Chacha Mwita walitupilia mbali ombi la Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji kupinga mawakili wenye tajriba ya juu James Orengo na Okong’o Omogen wakimtetea Jaji Mwilu.

Wakikataa kuwazuia Mabw Orengo na Omogen kumwakilisha Jaji Mwilu , majaji hao walisema “ DPP hakuwasilisha ushahidi kuonyesha jinsi wawili hao watakavyoathiri utenda kazi wake.”

Mawakili waliopinga Qureshi kuongoza mashtaka wakiongozwa na James Orengo (wa pili kushoto) na Okong’o Omogen (kati). Picha/ Richard Munguti

DPP alikuwa ameomba wawili hao wazuiliwe kumtetea Jaji Mwilu akisema yeye (haji) hufika mbele ya kamati ya bunge la Seneti kuhusu haki na dhuluma ambapo Orengo na Omogen ni wanachama.

DPP alikuwa amesema yeye hufika mbele ya kamati hiyo kuelezea utenda kazi wake na “ ikiwa anazingatia haki kwa washukiwa anaowafungulia mashtaka.”

“ Wakati DPP alifika mbele ya kamati hiyo ya bunge la Seneti hakuna suala la kesi ya Jaji Mwilu ilijadiliwa na kuwazuia mawakili hawa kumwakilisha naibu huyu wa CJ itakuwa ni kukandamiza haki zake,” majaji hao watano walisema.

Pia walisema DPP alishindwa kueleza jinsi utendakazi wake utaathiriwa na kushiriki kwa Mabw Orengo na Omogen katika kesi hiyo yaDCJ.