Wakimbizi 400 waliohepa Al-Shabaab wazidi kuishi kambini
NA KALUME KAZUNGU
ZAIDI ya wakimbizi 400 waliotoroka ghasia za Al-Shabaab Kaunti ya Lamu bado wanaendelea kuishi kwenye kambi ya wakimbizi ya Katsaka Kairu, tarafa ya Witu licha ya serikali ya kitaifa kuwaamuru kurudi makwao mwaka mmoja uliopita.
Wakimbizi hao wengi wao wakiwa ni kutoka vijiji vya Nyongoro na Maleli wanadaiwa kudinda kurudi vijijini mwao licha ya serikali kuimarisha usalama kwenye maeneo yao.
Badala yake, wakimbizi hao wamegeukia mashamba yaliyoko karibu na kambi hiyo ya Kastaka Kairu na kuendeleza unyakuzi wa ardhi bila mpango.
Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo mwishoni mwa juma pia ulibaini kuwa idadi kubwa ya wakimbizi tayari wameanza kujenga nyumba za kudumu kambini.
Baadhi ya waliohojiwa walishikilia kuwa bado hawajakuwa na imani na hali ya usalama vijijini mwao, jambo ambalo limewafanya kuendelea kuishi kambini.
Wengine walishikilia kuwa kamwe hawatabanduka kambini hadi pale serikali itakapowafidia hasara ya vyombo vyao, mimea na hata wakati waliopoteza wakati serikali ilipowalazimisha kuhamia kambini.
Bi Mariam Kachimbi ambaye ni mkimbizi kutoka kijiji cha Maleli aliitaka serikali kubuni kambi za jeshi na polisi kijijini mwao kabla ya wakazi kuamriwa kurudi makwao.
“Mimi sijaamini usalama tunaohakikishiwa mashambani kwetu. Ikumbukwe Maleli ni miongoni mwa maeneo ambayo Al-Shabaab wamekuwa wakilenga na kuchinja wakazi. Watujengee kambi za jeshi na polisi kwanza kabla ya kutuamuru kurudi vijijini,” akasema Bi Kachimbi.
Naye Bw Rama Kahindi alisema mazao yao mashambani yaliharibiwa yote na wafugaji wakati wakiwa kambini.
“Serikali ina jukumu la kutufidia kwanza kabla ya kutuamuru kurudi vijijini mwetu. Tukienda bila chochote gtutaishi vipi? Mimea yetu mashambani iliharibiwa. Vitu vyetu majumbani vikaibwa. Watufidioe kwanza ili tuweze kuanza maisha,” akasema Bw Kahindi.
Kwa upande wake aidha, Chifu wa eneo la Katsaka Kairu, Bw Kaviha Karisa alieleza wasiwasi kwamba hatua ya wakimbizi ya kuvamia na kunyakua ardhi za watu huenda ikapelekea vita miongoni mwa jamii eneo hilo.
Bw Karisa alisema tangu wakimbizi hao walipowasili Kastaka Kairu, eneo hilo limekuwa likishuhudia migogoro ya mara kwa mara ya wakazi wanaopigania ardhi.
Alisema kuna haja ya wakimbizi hao kurudi vijijini mwao kwani kuendelea kuishi eneo hilo huenda kukasababisha maradhi mbalimbali kuzuka hasa ikizingatiwa kuwa hakuna vyoo vya wakimbizi hao kutumia.
Alisema wakimbizi hao wamekuwa wakitumia vichaka ili kujisitiri.
“Tumeweka mikutano mara kadhaa ya kuwataka wakimbizi kurudi makwao lakini wamedinda. Wamegeuza mbinu ambapo wao huwarai wenzao waliorudi makwao kuja tena hapa kambini ili waendeleze unyakuzi wa ardhi. Hii ndiyo sababu idadi ya wakimbizi hapa Kastaka Kairu inaendelea kuongezeka kila kuchao badala ya kupungua,” akasema Bw Kaviha.
Mnamo Julai, 2017, serikali ya kitaifa iliamrisha wakazi wa vijiji vya Pandanguo, Jima, Poromoko, Kakathe, Maleli, Nyongoro na maeneo yote yanayokaribiana na msitu wa Boni kuhama vijijini mwao na kuishi kwenye kambi za Kastaka Kairu na Witu AIC ili kupisha serikali kuendeleza operesheni ya kuwasaka na kuwamaliza magaidi wa Al-Shabaab waliokuwa wakihangaisha wakazi hao mara kwa mara.
Serikali aidha iliwaamuru wakimbizi hao kurudi makwao mnamo Oktoba, 2017 baada ya usalama kuimarishwa kwenye vijiji husika.
Wanaoendelea kuishi kambini ni wale ambao wamekaidi amri hiyo