Habari Mseto

Wakulima pabaya serikali ikiagiza mahindi kutoka nje

August 27th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA BARNABAS BII

WAKULIMA kutoka Kaskazini mwa Bonde la Ufa sasa wanakodolewa macho na hasara kubwa baada ya mahindi yaliyoagizwa na serikali kutoka Uganda na Tanzania kujaa sokoni.

Kampuni za kibinafsi za kusaga mahindi nazo hazijaachwa nyuma, kwa kuwa zimekuwa zikinunua mazao hayo kutoka mataifa hayo mawili kwa bei ya chini ya Sh2,400 kwa kila gunia.

Serikali nayo imekosa kutoa magunia milioni 2 ya mahindi ya bei nafuu jinsi ilivyoahidi na kuchangia kampuni hizo kukimbilia mahindi kutoka nje huku wakulima wakiumia kwa kukosa soko la kuuza mazao hayo.

“Wakulima wa mahindi wanakodolewa macho na hasara kubwa kutokana na kushuka kwa bei ya mahindi huku mazao haya yakiletwa kwa wingi kutoka Tanzania na Uganda,” akasema mmoja wa wamiliki wa kampuni za kusaga mahindi Jackson Too.

Mwenyekiti wa Bodi ya Kuhifadhi Chakula(SFR) Dkt Noah Wekesa alisema Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao(NCPB) bado haijatoa maguni milioni 2 ya mahindi ya bei nafuu ambayo yatauzwa kwa Sh2, 700 kwa kila gunia la kilo 90 kutokana na ukosefu wa fedha.

Dkt Wekesa alithibitisha kwamba magunia kadha ya mahindi bado yataagizwa kutoka mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC) ili kuwawezesha Wakenya kumudu bei ya unga.

“Tumekuwa tukipokea mahindi zaidi kutoka Uganda kupitia miji ya mipaka ya Suam, Malaba na Busia. Vile vile tumeagiza mahindi kutoka Tanzania ambayo yatapitia Mombasa na Namanga ili Wakenya wasitatizike kwa kununua unga kwa bei ya juu kutokana na uhaba wa mahindi,” akasema Dkt Wekesa.

Kutokana na uagizaji wa mahindi kutoka Tanzania na Uganda, bei ya mahindi imeshuka kutoka Sh3,600 hadi Sh2,800 katika kaunti zote zinazopatikana Magharibi mwa Kenya.

Hata hivyo, Dkt Wekesa alishikilia kwamba kupanda kwa bei ya mahindi yanayotolewa na serikali kutoka kwa Sh2,300 hadi Sh2,700 kumechangiwa na uhaba ambao unaendelea kushuhudiwa hata baada ya uagizaji kutoka mataifa ya nje.

Nyingi za kampuni za kusaga mahindi kwa miezi michache iliyopita zimelazimika kusitisha shughuli na hata kuwatuma wafanyakazi wake likizoni kutokana na kupungua kwa kazi, hali iliyochangiwa na uhaba wa mahindi.