Wakulima wa mahindi sasa wahofia hasara
Na BARNABAS BII
WAKULIMA wa mahindi katika eneo la Bonde la Ufa, huenda wakapata hasara kubwa kufuatia mvua kubwa inayoendelea kunyesha.
Mvua hiyo imeharibu zao hilo na kutishia kusababisha uhaba wa chakula nchini.
Uharibifu huo pia umeathiri mifumo ya usafiri katika maeneo mengi nchini, hali ambayo imetatiza usafirishaji wa mavuno.
Mvua hiyo imetatiza shughuli ya kuvuna zao hilo iliyoanza mnamo Oktoba na inaendelea hadi mwezi ujao, huku Wizara ya Kilimo ikielezea hofu kwamba huenda isifikishe kiwango kilichopangiwa cha magunia 21 ya mahindi msimu huu. Hii ilisema ni kutokana na hasara inayosababishwa na kuoza kwa zao hilo.
“Mvua hiyo imesababisha zao kuozea shambani na kuvuruga faida iliyotarajiwa kutokana na bei nzuri msimu huu,” alisema, Bw Jackson Kosgei kutoka Moiben, Kaunti ya Uasin Gishu.
Wakulima hao walisema mvua imefanya kuwa vigumu kutumia mashine shambani huku mazao ambayo tayari yamevunwa yakikabiliwa na hatari ya kuoza kutokana na viwango vya juu vya unyevunyevu.
“Mvua imefanya vigumu kwa trekta zetu kufanya kazi shambani na kutulazimu kusimamisha shughuli za kilimo kwa kuwa hakuna mashine za kukausha mazao ambayo tayari yamevunwa na kufanya kuoza,” alisema Bw Wilson Kirwa kutoka Kibomet, kaunti ya Trans Nzoia.
Wiki iliyopita, baadhi ya wakulima waliisihi serikali kufungua mabohari ya Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB), ili kuwapa wakulima mitambo ya kukaushia nafaka.
Muungano wa Wakuzaji Nafaka (CGA) unasema kwamba serikali inapaswa kuwafadhili wakulima kukausha mahindi yao kwenye mabohari ili kuzuia uhaba wa chakula.