Habari Mseto

Wakulima wakerwa na serikali kuwacheleweshea fidia

December 17th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na KALUME KAZUNGU

WAKULIMA karibu 600 wa eneo ambako mradi wa nishati ya makaa ya mawe unanuiwa kujengwa kijijini Kwasasi, Kaunti ya Lamu sasa wanamtaka mwekezaji wa mradi huo na serikali kuu kuwaeleza iwapo mradi huo utafanyika au la.

Wakulima hao ambao wamekuwa wakisubiri fidia ya ardhi zao kwa zaidi ya miaka mitatu sasa, wameeleza kufadhaishwa kwao na kimya kinachoendelea kuhusiana na iwapo mradi huo utafaulu kuendelezwa eneo lao au la.

Katika mahojiano ya kipekee na Taifa Leo mjini Lamu Jumapili, wawakilishi wa wakulima hao walisema wameanza kukosa imani na serikali na mwekezaji kutokana na kile wanachodai kuwa ni kukosa huruma kufuatia muda mrefu na wakati uliopotezwa na wakulima bila kujiendeleza mashambani mwao.

Msemaji wa wakulima wa Kwasasi, Bw Abdulrahman Aboud, alisema wakulima wengi wanalazimika kuishi kwa umaskini baada ya kukosa kuendeleza kilimo mashambani mwao kufuatia ahadi za serikali na mwekezaji wa kiwanda hicho kwamba wangelipwa ridhaa ya ardhi zao.

Mradi huo wa nishati ya makaa ya mawe umekadiriwa kugharimu kima cha Sh200 bilioni.

Mradi huo uko chini ya usimamizi na ufadhili mkuu wa kampuni ya kibinafsi ya Amu Power na unalenga kuzalisha megawati 1,050 za umeme punde utakapokamilika.

Kufikia sasa tayari ekari 975 za ardhi zimetengwa kijijini Kwasasi ili kufanikisha mradi huo.

“Tunaiomba serikali na mwekezaji kujitokeza hadharani na kutueleza iwapo mradi upo au ilikatizwa. Tumechoka kukaa bila kuendeleza mashamba yetu. Tuliahidiwa kwamba tungelipwa mara moja ili kupisha kuendelezwa kwa mradi. Kimya ambacho kinaendelea kututisha. Watueleze kama mpango wa mradi kuendelezwa Kwasasi upo au haupo ili tulime mashamba yetu,” akasema Bw Aboud.

Bw Mohamed Omar alisema haielewi kwa nini serikali inakawia kuwafidia mashamba yao licha ya kwamba makadirio na usorovyeya wa ardhi husika tayari umefanywa na Tume ya Kitaifa ya Ardhi nchini (NLC) miaka kadha iliyopita.

“NLC tayari imefanya ukaguzi na kuwatambua wakulima halisi wanaofaa kufidiwa ardhi za Kwasasi. Pia imefanya tathmini na kuamua kiwango cha fidia kinachofaa kulipwa, ambapo kila ekari ni Sh 800,000. Kwa nini serikali inaendelea kukawia kutufidia? Watueleze iwapo tutafidiwa au la. Pia tujue iwapo mradi upo au haupo badala ya wahusika kunyamaza ilhali sisi tunaendelea kupoteza muda bure,” akasema Bw Omar.

Wakulima hao walitisha kwenda kortini kufikia Januari mwakani ili kudai haki yao ya fidia endapo serikali na mwekezaji itakuwa haijatekeleza shughuli ya kuwafidia kufikia wakati huo.