Wakulima waondolewa hofu ya uhaba wa mbegu za mahindi
Na GERALD BWISA
KAMPUNI ya mbegu nchini imewaondolea wakulima hofu kwamba kutakuwa na upungufu wa mbegu za mahindi kabla ya msimu ujao wa upanzi kuanza Kaskazini mwa Bonde la Ufa.
Wakulima wamekuwa na wasiwasi kwamba huenda wakakosa mbegu msimu ujao kutokana na ukame uliokithiri mwaka huu na kuathiri mavuno yao.
“Kukosa kupanda mahindi kwa wakati msimu huu ukianza kutakuwa na athari hasi kwenye mavuno. Tunahofu kwamba huenda tukawa na upungufu wa mbegu kutokana na ukame uliosababisha kuchelewa kwa upanzi huku wakulima wengine wakikosa kupanda kabisa,” akasema Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima Kaunti ya Trans Nzoia, Bw William Kimosong’.
Mkurugenzi wa Kampuni ya mbegu, Bw Azariah Soi hata hivyo alisema kwamba wakulima hawafai kuingiwa na wasiwasi kwa sababu wanatarajia mavuno mazuri kutokana na mahindi waliyopanda kwa ajili ya mbegu.
“Tuko na imani tele kwamba tutakuwa na mavuno mazuri kufikia mwisho wa msimu kwa sababu tumetunza vizuri mahindi tuliyoyapanda,” akasema Bw Soi.
Afisa huyo alitambua kwamba kuna haja ya taifa kutenga ardhi zaidi kwa ajili ya upanzi wa mbegu ili kuzuia upungufu.
“Naomba wizara ya kilimo kufanya kazi kwa pamoja na serikali ya kaunti ya Trans Nzoia ili kuhakikisha kwamba ardhi zaidi inatengewa kilimo cha mahindi ya mbegu,” akaongeza Bw Soi.
Aidha alishikilia kwamba kuanzishwa kwa kilimo cha miwa katika maeneo ya ukuzaji wa mahindi ni tisho kwa kuongezwa kwa kiwango cha mahindi kinachozalishwa.
“Kuanzishwa kwa kilimo cha miwa kaunti ya Trans Nzoia kutaathiri juhudi zetu za kumaliza wadudu na magonjwa yanayoathiri mahindi kwa kuwa mimea yote mawili inaathiriwa na magonjwa sawa,” akasema Bw Soi.
Gavana wa Trans Nzoia, Bw Patrick Khaemba amekuwa akiongoza juhudi za kuzima kilimo cha miwa eneo hilo akisema kitapunguza mavuno ya mahindi kila msimu.
“Tumeandikia Wizara ya Kilimo na kuomba kwa kilimo cha miwa kipigwe marufuku. Pia tunapanga kubuni sheria kama kaunti kuzima kilimo cha miwa,” akasema Bw Khaemba.