Wakulima watoa sababu ya wanyakuzi kumezea mate ardhi zao
NA KALUME KAZUNGU
WAKULIMA 542 ambao ardhi zao zilitwaliwa kwa ujenzi wa kiwanda cha nishati ya makaa ya mawe katika Kaunti ya Lamu wanasema kucheleweshwa kwa fidia ya ardhi zao kumetoa mwanya wa wanyakuzi kulenga ardhi hizo.
Wakulima hao kutoka kijiji cha Kwasasi, tarafa ya Hindi, wanasema tayari wamekuwa wakipokea vitisho kutoka kwa baadhi ya mabwenyenye wanaodai kumiliki ardhi hizo.
Licha ya usoroveya kutekelezwa na wamiliki halisi wa ardhi kutambuliwa takriban mwaka mmoja uliopita, kufikia sasa hakuna mkulima hata mmoja ambaye amepokea fidia kutoka kwa serikali.
Kulingana na maafikiano yaliyowekwa kati ya Tume ya Ardhi (NLC) na wakulima hao, kila mmiliki wa ardhi itakayotwaliwa kufanikisha ujenzi wa kiwanda hicho atafidiwa Sh 800,000 kwa kila ekari.
Wakiongozwa na Mwenyekiti wa wakulima wa Kwasasi, Bw Hussein Kombo, wakulima hao waliitaka serikali kuwafidia ardhi hizo haraka iwezekanavyo, wakidai huenda baadhi yao wakapokonywa ardhi na mabwenyenye.
“Tumesubiri fidia ya ardhi zetu kwa muda mrefu. Kazi yetu ni ya ukulima. Tangu ardhi zetu zilipotwaliwa, hakuna kilimo chochote kinaendelea hapa Kwasasi. Tulipwe fidia ili tutafute ardhi kwinghine ili tujiendeleze na familia zetu,” akasema Bw Kombo.
Mzee wa Mtaa wa Kwasasi, Bw Joseph Yeri, alisema ombi lao kwa serikali ni kwamba wasikie kilio chao cha muda mrefu na kuwafidia.
“Tumesubiri vya kutosha. Watupe fidia zetu. Wakiendelea kuchelewesha hizo fidia huenda watakaolipwa mwishowe wakawa si wamiliki halisi wa ardhi. Wanyakuzi wanazilenga hizi ardhi zetu,” akasema Bw Yeri.
Kiwanda hicho kinachokadiriwa kugharimu kima cha Sh 200 bilioni kiko chini ya udhamini wa kampuni ya kibinafsi ya Amu Power.
Kufikia sasa tayari jumla ya ekari 975 za ardhi zimetengwa kijijini Kwasasi ili kufanikisha mradi huo unaotarajiwa kuzalisha megawati 1,050 za umeme punde kitakapokamilika.