Habari Mseto

Wakuu wa KEBS kizimbani kwa jaribio la kuua Wakenya

June 26th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na Richard Munguti

MAAFISA wakuu katika Shirika la Ubora wa Bidhaa (KeBS), akiwemo Mkurugenzi Mkuu, Charles Ogega Ongwae na maafisa wengine, Jumatatu walishtakiwa kwa jaribio la kuwaua wakazi wa kaunti za Narok na Uasin Gishu.

Washukiwa hao tisa walidaiwa kutenda kosa hilo kwa kuwauzia wakazi hao mbolea iliyokuwa na madini ya Zebaki (Mercury), ambayo ina madhara kwa afya ya binadamu. Korti iliagiza wengine 10 wakamatwe.

Washukiwa hao pia walikabiliwa na shtaka la kula njama za kuibia Serikali Sh882 milioni kwa kuruhusu kampuni isiyo na ujuzi kuchapisha stempu feki za KeBS.

Upande wa mashtaka ukiongozwa na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Bw ALexander Muteti akishirikiana na viongozi wengine saba wa mashtaka, walipinga washtakiwa kuachiliwa kwa dhamana wakisema mashtaka dhidi yao ni mabaya kwa vile makosa wanayodaiwa kutenda yanahatarisha maisha ya mamilioni ya Wakenya.

Hakimu Mwandamizi Bw Kennedy Cheruiyot aliamuru Mabw Prathap Singh, Rajah Sunder Singh, Arui Prathan Singh, Sam Prasad, Asir Prathan Singh, Susela Rajah, Ponmani Prasadd na Ramachadran Ntaarajan watiwe nguvuni na kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka.

Washukiwa hao 10 ni pamoja na wawakilishi wa kampuni ya kampuni ya Madras Security Printers Limited walioagizwa washikwe na kufikishwa kortini.

“Washtakiwa 10 ambao ni raia wa kigeni hawajakamatwa. Naomba korti itoe kibali cha kuwatia nguvuni popote walipo,” aliomba Mw Muteti.

Bw Ongwae alishtakiwa pamoja na Mabw Erik Chesire Kiptoo (meneja wa ukadiriaji ubora- KeBS), Bw Peter Kinyanjui Ndung’u (meneja mkaguzi KeBS Bandari ya Mombasa), Bw Martin Muswanya Nyakiamo (msimamizi wa KeBS kanda ya Pwani), Bw Pole Mwangeni (afisa wa afya Bandari ya Kilindini) na Bw Benson Oduor Ngesa (ajenti wa uingizaji bidhaa nchini).

Washtakiwa hawa tisa walikanusha kuwa walinuia kuwaua wakazi wa Narok na Eldoret sumu kwa kuruhusu kilo 5,846,000 za mbolea yenye madini ya Mercury kuuziwa wakulima wakijua haikufaa kwa matumizi ya binadamu.

Mbali na kashfa ya Mbolea Bw Ongwae alishtakiwa kwa kashfa nyingine ya kuruhusu kampuni ya Madras Security Printers Private Limited kuchapisaha Stempu feki za ukadiriaji wa ubora wa bidhaa.

Bw Ongwae alishtakiwa na maafisa wengine ambao ni Erick Ochieng Onyango,, Bw Erick Kimutai Kirui, Bi Christine Jepchieng Bowen, Robin Shake, Rhoda Olesi Kirui na Bw John Murungi Rukaria.

Bw Muteti alipinga ombi la washtakiwa kuachiliwa kwa dhamana akisema watavuruga mashahidi ikitiliwa maanani mashahidi wengi ni wadogo wa washtakiwa hao katika Shirika la KeBS.

Bw Muteti alisema mbali na kesi Polisi wanaendelea kuchunguza bidhaa nyingine feki ambazo zimeingizwa nchini na kuuziwa wananchi.

Hakimu aliwaachilia kwa dhamana kali ya jumla ya Sh23 milioni kila mmoja.