Habari Mseto

Walia waliozua fujo wako huru

November 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na SHABAN MAKOKHA

BAADHI ya viongozi wa kisiasa katika eneo la Magharibi mwa nchi wanamtaka Inspekta Mkuu wa Polisi, Bw Hillary Mutyambai, awakamate watu waliohusika na vurugu wakati wa uchaguzi mdogo wa Kibra.

Viongozi hao wamesema wanashangazwa na jinsi tume ya uchaguzi na mipaka imeendelea kukimya kuhusu jambo hilo ambalo liliepeperushwa wazi kwenye vyombo vya habari.

Mbunge wa Tongareni, Dkt Eseli Simiyu na mwenzake wa Mumias, Bw Benjamin Washiali, wamemtaka Bw Mutyambai afanye hima na kuhakikisha kuwa haki inatendeka na visa sawia vinakomeshwa.

Wameonya kwamba ikiwa wahusika hawatakamatwa na kushtakiwa, huenda visa kama hivyo vikaongezeka mara dufu wakati wa uchaguzi mkuu ujao.

Dkt Simiyu alisema vurugu zilianza kushuhudiwa wakati wa kampeni za mapema ambapo wafuasi wa ANC na Ford Kenya walifurushwa kutoka kwa mikutano iliyokuwa imepangwa.

“Lazima tuwajibike jinsi ambavyo tunaendesha uchaguzi humu nchini. Vurugu zilishuhudiwa Kibra tangu wakati wa kampeni na kufikia sasa polisi pamoja na tume ya IEBC wamezidi kuwa kimya,” akasema Dkt Simiyu.

Katibu huyo mkuu wa Ford Kenya aliongeza kuwa swala hilo linapaswa kushughulikiwa kwa haraka ili kuonyesha tofauti na miaka mingine.

Kwenye uchaguzi huo, Imran Okoth wa chama cha ODM alishinda kwa kura 24, 636 akifuatwa na Mac Donald Mariga wa Jubilee, aliyepata kura 11, 230.

Uchaguzi huo ulidhihirika kupima nguvu kinara wa ODM Raila Odinga na Naibu Rais, Dkt William Ruto.Wakati huo, mbunge wa Kimilili, Bw Didmus Barasa, alicharazwa makofi huku kofia yake ikitolewa kichwani na kutupwa.