Habari Mseto

Walichoandika baadhi ya watumiaji mitandao ya kijamii kumhusu Ken Okoth

July 27th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MARY WANGARI

WATUMIAJI mitandao ya kijamii mbalimbali wameendelea kumwomboleza Mbunge wa Kibra Bw Ken Okoth aliyefariki Ijumaa kutokana na maradhi ya saratani ya utumbo.

Bw Okoth aliyekuwa akiugua saratani ya utumbo Alhamisi aliwahiwa katika Nairobi Hospital baada ya hali yake kuzorota zaidi, lakini akafariki Ijumaa.

Alikumbana na kifo chake akiwa na umri wa miaka 41.

Awali, familia yake ilifunguka kuhusu maagizo ya mwisho aliyowaachia kabla ya kifo chake ambapo mbunge huyo aliwaomba madaktari wasimweke kwenye mitambo ya kuwezesha uhai endapo angezidiwa.

Hata hivyo, madaktari hawakuwa na hiari ila kumweka kwenye mashine viungo vyake vingi viliposhindwa kufanya kazi.

Kifo cha Mbunge huyo wa Kibera kilihuzunisha na kuvunja nyoyo za Wakenya ikizingatiwa kilitojokea takribani wiki tatu tu baada ya kifo cha Afisa Mkuu Mtendaji wa Safaricom Bob Collymore aliyeaga dunia akiwa na umri wa miaka 61 kutokana na saratani ya damu.

Kufuatia kifo cha Bw Okoth, watumiaji mtandao wa kijamii wa Twitter wameelezea hisia zao na kumwomboleza kupitia #RIPHonKenOkoth .

Baadhi ya hisia zao ni kama zifuatazo:

Charles Nyerere: “Lau kifo kingewauliza wananchi kujitolea kutoa orodha ya viongozi katika taifa hili, Ken bado angekuwa hai!”

Kevin Kathurima: “Sijawahi kumwonea huruma mwanasiasa lakini kwa mara ya kwanza nimehuzunishwa na kifo cha mheshimiwa. Kwa kweli alikuwa shujaa wangu.”

Mtumiaji mwingine wa mtandao huo, Brian Mutiga ameandika kwamba taifa la Kenya limepoteza kiongozi mzuri.

“Ken Okoth alikuwa na atasalia kuwa kiongozi bora zaidi ya wote kwangu, mwenye bidii na kiongozi halisi aliyewatakia watu mema. Tumempoteza kiongozi mkuu. Safiri salama,” akaandika Brian Mutiga.

MiracleBaby naye hajaachwa nyuma.

“Mbona ni viongozi wazuri tu wanaotuacha na majambazi wanasalia kuwakamua Wakenya? Ken Okoth ulikuwa mzalendo halisi! Shujaa. Ulikuwa na mawazo mema katika hali zote na hilo pekee ni baraka,” amesema MiracleBab.

Mtumiaji mwingine kwa jina Michael Barasa ameandika: “Hata mautini bado unapendwa na utapendwa milele. Ken Okoth umegusa nyoyo za watu wengi sana watakaokukumbuka maisha yao yote. Hatusemi kwaheri milele ila tu kwa sasa. Naomba upate amani na upumzike popote ulipo.”

“Nimeshtuka na kuhisi uchungu. Tumempoteza kiongozi halisi mwenye maono, binadamu asiye na ubinafsi aliyetuonyesha uongozi wa kweli ni nini. Hatujawahi kumwona anayefanana nawe Kibra. Ken ameacha historia,” akaandika Sheenaz Ali Zaids.