Walimu wa Kenya wapata tuzo za UN, AU
Na COLLINS OMULO na FAITH NYAMAI
WALIMU wawili wa humu nchini wamepata tuzo ya kimataifa wiki hii kwa kazi nzuri na kwa kuwasaidia wanafunzi kuweza kujisaidia katika mazingira wanamoishi.
Mwalimu Bora Duniani Peter Tabichi ametunukiwa heshima nyingine kwa kutawazwa na Umoja wa Mataifa (UN) kama Mkenya Bora Mwaka wa 2019.
Naye Mwalimu wa Masomo ya Hisabati na Kemia katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Asumbi Erick Ademba Jumatano alikuwa miongoni mwa walimu watatu kutoka Afrika ambao walipewa tuzo ya Umoja wa Afrika (AU) kwa utendakazi wao wa mzuri.
Bw Ademba alipewa cheti na zawadi ya dola 10,000 za Amerika (sawa na Sh1 milioni) katika sherehe iliyofanyika katika Makao Makuu ya AU jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Walimu wengine waliozawidiwa ni Augusta Lartey kutoka Shule ya Upili ya Presbyterian ncjhini Ghana na Gladys kutoka Uganda.
Mnamo Machi mwaka huu Tabichi aliandikisha historia kwa kuwa mwalimu wa kwanza kutoka Afrika kushinda tuzo ya Mwalimu Bora Ulimwenguni kwa mara ya kwanza miaka mitano baada ya tuzo huyo kuanzishwa. Alitia kibindoni Sh100 milioni .
Kwa kutambuliwa na UN kama Mtu Bora Mwaka huu, Mwalimu Tabichi amejiunga na orodha ya watu wachache ambao wamewahi kutawazwa Mtu Bora wa Mwaka na umoja tangu mwaka wa 2002.
Tabichi alituzwa kwa kielelezo cha umuhimu wa elimu na thamani na heshima ya taaluma ya elimu kama chombo ya kukabiliana na changamoto za maisha.
Akipokea tuzo hiyo, Tabichi ambaye ni mwalimu wa Hisabati na Fizikia katika Shule ya Upli ya Kerika katika Kaunti ya Nakuru alitoa wito kwa serikali kuhakikisha kuwa inaipa kipaumbele elimu ya mtoto wa kike.
Na Bw Ademba, na wenzake wawili, walituzwa kwa kuwasaidia watoto kutimiza matamanio yao, kutoa mafunzo yenye ubora na kupalilia mienendo hitajika shuleni kati ya mambo mengine.
Akiongea baada ya kupata tuzo hiyo, Bw Ademba, alisema itaimarisha heshima na taadhima ya ualimu barani Afrika.
“Tuzo hii pia itawatia shime walimu kuwa wabunifu. Hii ni kando na kuimarisha hadhi ya kazi hii kwa sababu sasa walimu barani Afrika watahisi wanathaminiwa,” akasema Bw Ademba.
Mwalimu huyo aliwasili nchini Alhamisi na kulakiwa kwa nderemo, vifijo na furaha tele na maafisa wa Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA), Nairobi.
Akiongea katika hafla hiyo Beatrice Njenga, ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Elimu katika AU, alisema kuwa tuzo hiyo ya walimu ni muhimu kama chombo ambacho kitachangia ufanisi wa Agenda ya 2063 ya AU.
Vile vile, akaeleza, tuzo hiyo inafanikisha kufikiwa kwa Mkakati wa kustawisha Elimu barani Afrika (CESA).
“Tuzo hii itaimarisha hadhi ya heshima ya Mwalimu Afrika katika ngazi zote; kuanzia chekechea hadi chuo kikuu, na hata vyuo vya kiufundi (TVET). Pia itawapa wanafunzi mshawasha na msukumo wa kuteua ualimu kama taalamu ya kwanza vyuoni,” akaongeza Bi Njenga.