• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Walimu wa shule za kibinafsi walia kunyimwa malipo ya Machi

Walimu wa shule za kibinafsi walia kunyimwa malipo ya Machi

By GEOFFREY ANENE

Chama cha Walimu kutoka Shule za Kibinafsi za kaunti ya Nairobi kimethibitisha kupokea malalamishi mengi kutoka kwa walimu kuhusu waajiri wao kutowapatia mishahara ya Machi ama kuikata, huku makali ya virusi hatari vya corona yakiendelea kushuhudiwa nchini Kenya na kote duniani.

Katika mahojiano Jumapili, chama hicho kilicho na wanachama 728, kilieleza Taifa Leo kuwa kimewasilisha kesi hizo za malalamishi kwa Afisi za Leba katika maeneo wanayotoka ili hatua zifaazo zichukuliwe.

“Hali hii inatokana na baadhi ya shule kukosa kukusanya asilimia 100 ya karo za shule, ingawa pia kuna shule ambazo wamiliki wameamua tu kutolipa walimu,” anasema katibu wa chama hicho, Barasa Chivile.

Kesi nyingi, afisa huyo anasema, hutatuliwa kwa haraka, hasa zinazohusu mfanyakazi ama mwalimu kuachishwa kazi bila notisi kinyume na mkataba unaovyosema.

Hata hivyo, aliongeza, “Ulipaji wa mishahara ya Machi inajitokeza kuwa changamoto kubwa. Shule nyingi zimefungwa na kupata jibu imekuwa kibarua kigumu.”

Mwalimu mmoja kutoka akademia ya Smart Kids mtaani Kariobangi South Civil Servants, ambaye hakutaka kutajwa, alithibitisha hali ilivyo. “Ni masikitiko makubwa kuwa mshahara wa Machi haukuingia kabisa,” anasema.

Mwalimu mwingine kutoka shule za Nairobi Rabbani alifichua kuwa yeye alipata nusu ya mshahara wake. Hata hivyo, alikuwa na matumaini mambo yatakuwa mazuri Mei.

Aliongeza, “Wanafunzi wanapokuwa nyumbani, hakuna karo ya shule inalipwa na kwa hivyo, shule nyingi za kibinafsi zinashindwa kulipa wafanyakazi wao.”

Huku walimu walioajiriwa na serikali wakifurahia kupokea mishahara yao kama kawaida, hali ya walimu katika shule za kibinafsi kote nchini haitarajiwi kuwa tofauti na ile ya Nairobi.

Mnamo Machi 15, Rais Uhuru Kenyatta aliamrisha taasisi zote za elimu zifungwe ili kuzuia uenezaji wa maambukizi ya virusi vya corona, ambavyo vimeua watu 13 nchini Kenya na visa 262 kuripotiwa. Vimehangaisha dunia nzima tangu visambae kutoka mjini Wuhan nchini Uchina mapema mwaka huu, huku kila sekta ya maisha ikiathirika.

You can share this post!

Corona: Maduka ya Eastleigh yafungwa

Icardi kujaza pengo la Diego Costa Atletico

adminleo