Habari Mseto

Walimu walalamikia kukatwa mishahara bila taarifa

October 1st, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na Lucy Mkanyika

WAKUFUNZI wa chuo cha Coast Institute of Technology mjini Voi, Kaunti ya Taita Taveta, wamelalamikia kukatwa mishahara yao bila kufahamishwa na mwajiri wao.

Walimu hao zaidi ya 85 walidai kuwa mishahara yao ya Septemba ilikatwa kwa kati ya Sh12,000 na Sh40,000.

“Hatujui kwa nini serikali ilikata mishahara yetu. Linalotuudhi ni kuwa hatukupewa taarifa yoyote ya kutueleza kuwa tumehamishwa ama tutapunguziwa mshahara,” akasema Bw Gabriel Odhiambo.

Wakiongea chuoni humo, walisema walishangazwa na hatua hiyo na kukisia kuwa huenda ikawa walihamishwa kutoka kwa Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) hadi ile ya watumishi wa umma (PSC).

Mahakama ya uajiri ilikuwa imeagiza mchakato wa kuhamisha walimu wa vyuo vya kiufundi nchini kutoka kwa TSC hadi kwa PSC usitishwe. Amri hiyo ilitolewa baada ya walimu watano kushtaki serikali kutokana na hatua ya wao kuwahamishwa mnamo Septemba 19.