Habari Mseto

Walimu walia kulemewa na mtaala mpya wa mafunzo

June 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na Oscar Kakai

WALIMU katika Kaunti ya Pokot Magharibi wamemlalamikia Waziri wa Elimu, Prof George Magoha kwa kuharakisha kutekeleza mfumo mpya wa elimu wa 2-6-3-3.

Akizungumza kwa niaba yao, Katibu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT) tawi la eneo hilo, Bw Martin Sembelo alisema si vyema walimu kulazimishiwa mfumo huo kwani hawajapokea mafunzo bora.

Kulingana naye, eneo hilo bado linakumbwa na ukosefu wa vifaa vya elimu, uhaba wa walimu na mafunzo duni ya walimu kuhusu mfumo huo.

Alisema walimu wakuu katika kaunti hiyo wamelalamikia pia changamoto za miundomsingi shuleni.

“Tuna uhaba wa walimu 3,000 katika kaunti hii. Kuna mapengo mengi kwenye mfumo huo. Hatuwezi kuwafanyia watoto wetu majaribio kuhusu mfuno ambao hauna mwelekeo,” alisema.

Maafisa wakuu wa KNUT walikutana Nairobi Jumatano na kusema wako tayari kushauriana na serikali kuhusu mfumo huo, ijapokuwa masharti yao hayajabadilika.