Habari Mseto

Walimu wanaokwepa kazi kunaswa na BVR

July 16th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na ANITA CHEPKOECH

VISA vya walimu kukosa kufika shuleni mara kwa mara katika Kaunti ya Bomet huenda vikadhibitiwa endapo mpango wa serikali ya kaunti wa kuwatambua kwa kutumia alama za vidole utatekelezwa.

Kuwatambua walimu kielektroniki kwa kutumia alama za vidole (BVR) ni miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa na jopokazi lililokuwa likichunguza jinsi ya kuboresha kiwango cha elimu katika shule za sekondari na vyuo anuai kwenye kaunti hiyo.

Jopokazi hilo lilizinduliwa na Gavana Joyce Laboso miezi mitano iliyopita ili kuchunguza kiini cha wanafunzi kufanya vibaya katika mtihani wa kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) wa 2017.

Kamati hiyo ilinyoonyeshea kidole cha lawama uhaba wa walimu, miundomsingi duni ya kufundishia na walimu na wanafunzi kukosa kufika shuleni mara kwa mara kuwa miongoni mwa changamoto zinazokumba elimu katika kaunti hiyo.

Ripoti hiyo iliyokabidhiwa jana kwa Dkt Laboso na jopokazi la washiriki 19 lililoongozwa na Dkt Kirui Kipngetich, linapendekeza kuboreshwa kwa miundomsingi shuleni na kwenye vyuo anuai.

Hata hivyo, haijulikani jinsi serikali ya Kaunti ya Bomet itatekeleza ripoti hiyo kwani elimu ya msingi na sekondari inasimamiwa na serikali ya kitaifa. Serikali ya kitaifa inasimamia elimu ya chekechea pekee.

Lakini, serikali ya kaunti ilisema mapendekezo hayo yatatekelezwa kwa ushirikiano na serikali ya kitaifa. Tayari serikali ya kaunti ya Bomet imekamilisha ujenzi wa shule 75 za chekechea katika awamu ya kwanza.

Shule nyingine 27 zinatarajiwa kujengwa kwenye wadi mbalimbali katika awamu ya pili.