Walioasi ugaidi wasaidiwe – DPP
Na MOHAMED AHMED
UKOSEFU wa mpango murwa wa kuwarekebisha tabia na kuwarudisha kwenye jamii waliokuwa wamejiunga na makundi ya kigaidi, kunazorotesha vita dhidi ya uhalifu huo.
Hili liliibuka jana huku serikali ikifichua mbinu mpya zinazotumika na magaidi kuingiza vijana kwenye makundi yao.
Ilifichuka pia kuwa, licha ya Mombasa kuwa miongoni mwa maeneo yenye visa vingi vya kuhusiana na masuala ya ugaidi, hakuna hata kituo kimoja cha kurekebisha tabia kwa wale wanaoujinasua kutoka kwenye makundi hayo.
Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Noordin Haji alieleza kuwa kushuka kwa maadili katika jamii kumechangia pakubwa vijana kuingizwa kwenye makundi hayo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango wa kupambana na misimamo mikali katika hoteli ya Pride Inn, jijini Mombasa, Bw Haji alisema ukosefu wa mpango wa kutatua shida za vijana wanaorudi kutoka Somalia na kwingineko kunakosesha mwelekeo vita hivyo.
“Tumeona ongezeko la talaka, hali inayochangia vijana wetu kuingizwa kwenye makundi hayo kwa urahisi,” akasema Bw Haji.
Alieleza kuwa kuna haja ya kuondoa kasumba kuwa kila Muislamu ni gaidi, na kusisitiza kuwa Kenya ni nchi huru ambayo inazingatia umuhimu wa dini.
“Kama Waislamu tusipeane nafasi kwa wale wenye nia ya kuharibu jina la dini hii. Ni lazima tusimame wima ili kuondoa tatizo hili la ugaidi, ambalo linaleta picha mbaya kwetu,” akasema.
Mkurugenzi wa shirika la Haki Afrika, Hussein Khalid alisema kuwa, kuhusishwa kwa jamii ni njia kuu ya kupambana na magaidi ambao hueneza imani potovu miongoni mwa wananchi, hasa vijana.