Waliochelewa kulipa kodi watupwa nje Juja
Na LAWRENCE ONGARO
WAKAZI wa kijiji cha Witeithie, Juja, Kaunti ya Kiambu, wameanza kufurushwa kutoka kwa nyumba zao baada ya kutolipa kodi.
Katika jumba moja la Limpopo, eneo hilo wapangaji wamekatiwa maji, umeme, na hata milango za nyumba zao kung’ olewa ili wahame.
Lucy Njeri ambaye ameishi kwa ploti hiyo kwa zaidi ya miaka minne anasema landilodi wake amewaweka katika hali tatanishi kwa sababu hawawezi kwenda kufanya kibarua chao kwa kuhofia mali yao kuibwa.
“Ama kweli tumefanyiwa unyama na mwenye nyumba na tayari tulimweleza kuwa tutamlipa kabla ya tarehe 10 mwezi huu wa April , 2020,” alisema Bi Njeri.
Alisema kwa wakati huu hana kazi maalum kwa sababu alikuwa anauza Sokoni na sasa hayuko huko.
Walisema sasa wanahofia kuambukizwa corona kwa sababu wamekosa maji na maisha ni magumu kwao.
Mpangaji mwingine, Bw Ambrose Odero anasema ameishi katika ploti hiyo miaka minne na alipatwa na mshangao alipopata mlango wa nyumba yake ukiwa umevunjwa na kung’ olewa.
” Jambo hilo limenitia kiwewe zaidi kwa sababu sasa siwezi kwenda kufanya kibarua change cha kila Siku nikihofia kuibiwa mali yangu,” alisema Bw Odera.
Alisema baadaye pia hawana umeme na maji jambo ambalo ni habari kwa usalama na afya yao.
Aliitaka serikali kuingilia kati na kuchukua hatua Kali kwa landilodi huyo ambaye ameonyesha ukatili wake kwa wapangaji.
Alisema hali ya ujambazi umezidi eneo hilo na kwa hivyo hata kulala usiku ni shida.
Landilodi wa ploti hiyo ambaye hakujitaja jina lake anasema wapangaji hao wamemzoea vibaya na kwa hivyo hangewapa nafasi zaidi.
” Wapangaji ni walewale ambao hata ukiwafanyia jambo lipi bado watakuletea shida zao,” alisema mwenye ploti hiyo.
Wakazi wengi wa kijiji hicho wanaitaka serikali kuu kuingilia kati ili kuwaokoa kutoka kwa masaibu haya mazito.