Walioingiza wasichana wa Nepal nchini kunengua viuno waachiliwa
Na RICHARD MUNGUTI
MMILIKI wa kilabu kimoja maarufu jijini Nairobi wanaoshtakiwa kuwaigiza nchini wasichana tisa kuwachezea densi wateja wao waliachiliwa Jumatano kwa dhamana ya Sh2milioni pesa tasilimu.
Mabw Shaikh Furoan Hussain na Abdul Waheed Khan waliokanusha mashtaka manne dhidi yao ya ulanguzi wa binadamu na kukandamiza haki za wasichana hao kwa kuchukua pasipoti zao na kuzificha kinyume cha sheria walichiliwa na hakimu mkuu mahakama ya Nairobi Bw Francis Andayi.
Walikanusha mashtaka ya ulanguzi wa bindadamu kisha wakili Cliff Ombeta akaomba waachiliwe kwa dhamana.
Wawili hao walishtakiwa kuwa kati ya Feburuari 19 na Julai 9 mwaka huu wakishirikiana na watu wengine ambao hawajafikishwa mahakamani waliwaingiza raia mmoja wa Pakistan na raia wanane wa Nepal humu nchini kwa njia ya undanganyifu.
Shtaka lilisema kuwa wasichana hao waliokamatwa wakicheza densi katika kilabu hicho kujipatia riziki.
Kiongozi wa mashtaka Bw Solomon Naulikha alimweleza hakimu kuwa wawili hao walitwaa pasipoti za wasichana hao tisa kwa lengo la kuficha idara ya uhamiaji uraia wa wasichana hao.
Washtakiwa hao walikabiliwa na shtaka lingine la kuwasaidia wasichana hao kuingia humu nchini kinyume cha sheria za idara ya uhamiaji.
Shtaka lingine la kuwaficha wasichana hao kinyume cha sheria katika mtaa wa Parklands Nairobi.
“ Upande wa mashtaka unapinga washtakiwa hawa wakiachiliwa kwa dhamana ndipo kiini chao kuwaingiza wasichana hawa hapa nchini kijulikane,” akasema Bw Naulikha.
Alisema adhabu ya makossa waliyofanya washtakiwa ni kali na wakiachiliwa kwa dhamana washtakiwa watatoroka.
Aliomba mahakama iwazuilie washtakiwa gerezani hadi kesi inayowakabili isikizwe na kuamuliwa.
Bw Ombeta alisema dhamana ni haki ya kila mshtakiwa na kumsihi hakiku awaachilie washtakiwa kwa dhamana.
“ Washtakiwa ni raia wa Kenya. Mahala pao pa kuishi na kufanyakazi panajulikana,” alisema Bw Ombeta.
Alieleza mahakama mshtakiwa anaweza kunyimwa dhamana ikiwa ushahidi umewasilishwa kuthibitisha atavuruga utekelezaji wa haki.
“ Naomba hii mahakama iwaachilie kwa dhamana kwa vile ni haki yao ya kikatiba,” alirai Bw Ombeta.
Bw Andayi aliamuru washtakiwa wazuiliwe gerezani akisubiri kutoa uamuzi wa ombi lao ya dhamana.