Habari Mseto

Wamalwa awataka viongozi waunge mkono vita dhidi ya ufisadi nchini

January 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na OSCAR KAKAI

WAZIRI wa Ugatuzi Eugene Wamalwa amewataka magavana na wabunge kusaidia kupigana na jinamizi la ufisadi nchini.

Akiongea wikendi katika shule ya Chemororoch, kaunti ya Pokot Magharibi ambapo alijiunga na viongozi wengine kukagua miradi ya maendeleo, Bw Wamalwa alisema kuwa ufisadi umesalia kuwa tishio kubwa kwa ugatuzi.

“Serikali kuu pekee haiwezi kufaulu vita dhidi ya ufisadi. Tunafaa kuwa na serikali za kaunti kukabiliana na shida hiyo mara moja,” alisema.

Bw Wamalwa alitaja ufisadi kama tishio kubwa kwa ugatuzi huku akitilia shaka kuhusu namna unavyotatuliwa.

Alisema kuwa anamuunga kwa dhati Rais Uhuru Kenyatta kuhusu juhudi zake mpya kupigana na shida hiyo.

“Tunafaa kushirikiana na kuona kuwa tunaanzia kwa kiwango cha familia kwa kuwashauri na kuwahimiza watoto kuwa na nidhamu kisha tuweke kwa serikali zetu za kaunti,”alisema.

Bw Wamalwa aliwataka magavana kukabiliana na maovu ya ufisadi ili kuimarisha maendeleo huku akionya dhidi ya matumizi mbaya ya fedha za umma ambazo zinanuiwa kuimarisha huduma .

“Ufisadi bado ni adui mkubwa wa ugatuzi. Tunataka kumaliza kabisa shida hii. Tunataka kuona vita dhidi ya ugatuzi vikikumbatiwa kwenye kaunti. Tunataka fedha ambazo zinatumwa kwenye kaunti kuimarisha maisha ya wakenya,” akasema Bw Wamalwa.

Bw Wamalwa alisema kuwa magavana lazima kuweke mikakati maalumu na kuunga mkono Rais Kenyatta kupigana na ufisadi nchini.

“Serikali kuu imeonyesha njia mwafaka na magavana pamoja na wabunge wanafaa kuhakikisha kuwa hawaruhusu ufisadi kwenye kaunti,”alisema.

Aliongeza kusema kuwa kaunti zitawaajibika ikiwa mipango maalumu haziwekwi kabla ya miradi kutekelezwa.

Waziri huyo alisisitiza umuhimu wa fedha huonekana kwenye matumizi bora na serikali za kaunti.

Bw Wamalwa aliongeza kusema kuwa sheria za uekezaji na matumizi ya fedha inafaa kufuatwa kikakamilifu.