• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Wamiliki wa shule za kibinafsi waionya Serikali

Wamiliki wa shule za kibinafsi waionya Serikali

Na WINNIE ATIENO

WAMILIKI na wawekezaji wa shule za kibinafsi nchini wameonya Serikali isithubutu kuwaajiri walimu wanaohudumu katika shule za kibinafsi.

Wakizungumza Jumatano wakati wa kufunguliwa kwa kongamano la kila mwaka la chama cha shule za kibinafsi nchini, wamiliki hao walisema kuna walimu wengi waliohitimu kutoka vyuo vya mafunzo ya elimu au vyuo vikuu ambao hawana ajira.

Mwenyekiti wa muungano wa shule za kibinafsi, Bi Mutheu Kasanga, alisema mpango wa kuajiri walimu 88,000, wengi wakiwa wale wa shule za kibinafsi au wenye tajriba ya miaka mitano, haufai.

“Tuliona katika vyombo vya habari tukashtuka kuwa serikali inapania kuajiri walimu 88,000. Hali hii itatuletea taharuki kwa kuwa hawa walimu wanatoka katika shule za kibinafsi. Tutakosa walimu waliohitimu kabisa,” akasema.

Mabwenyenye wa shule hizo walisema serikali itawaharibia biashara yao endapo wataajiri walimu hao, jambo ambalo litasababisha upungufu mkubwa wa walimu.

Bi Kasanga alisema walimu wa shule za kibinafsi wanabaguliwa katika mafunzo ya silabasi mpya inayotarajiwa kuanzishwa mwaka 2018.

“Kama serikali inatujali basi waajiri walimu waliomaliza ualimu kutoka vyuo vikuu au katika taasisi za elimu nchini badala ya wale wenye tajriba ya miaka mitano au zaidi.

Tunajua wataajiri wale kutoka shule za kibinafsi. Kazi yetu ni kupanda wengine wanavuna,” akasema Bi Kasanga akiwahutubia wawekezaji hao katika hoteli ya Prideinn, Mombasa.

Alisema shule za kibinafsi huajiri walimu waliohitimu.

“Tukishawaajiri tunawapa mafunzo na wanapopata tajriba ya kutosha serikali inawavizia. Hatupingi kuwa serikali inalipa bora zaidi kando na marupurupu mengine lakini msilemaze sekta ya kibinafsi,” akasihi.

Bi Kasanga alisema walimu wote wanaoajiriwa katika sekta ya kibinafsi wamehitimu na hata kusajiliwa na tume ya kuajiri walimu nchini, TSC.

“Serikali inatutumia vibaya sana sisi tunakuza walimu, wao wanawachukua tu. Tunajitayarisha kwa upungufu mkubwa wa walimu baada ya serikali kutangaza nafasi hizo. Kuna zaidi ya shule 12,000 za kibinafsi zinazoajiri zaidi ya walimu 100, 000,” akaongeza.

Mnamo Jumanne, Serikali ilitangaza kuwa itaajiri walimu 88,000 kwa gharama ya Sh26 bilioni ili kukabiliana na uhaba wa walimu 104,821 nchini.

Wakati huo huo, alisema silabasi mpya inakumbwa na changamoto kadha wa kadha ikiwemo mafunzo ya walimu ambao watanao wanafunzi chini ya silabasi hiyo.

Bi Kisanga alisema shule za kibinafsi zinabaguliwa katika kupewa mafunzo kwa walimu wao wakijitayarisha kwa silabasi hiyo mwaka ujao.

 

You can share this post!

Afueni kwa vijana bunge kuwaondolea visiki vya kupata ajira

GWIJI WA WIKI: Mwalimu, mshairi na mwandishi chipukizi

adminleo