Wanachama wa Urithi Housing Co-operative wapewa mwongozo
Na LAWRENCE ONGARO
CHAMA cha ushirika cha Urithi Housing Co-operative Society Ltd kimezindua mpango wa kuwahamasisha wanachama wake tangu kipindi cha mwezi mmoja ambao umepita.
Lengo kuu hasa ni kuwajulisha wanachama wake jinsi watakavyokuwa wakiendesha miradi yao kutoka mwaka wa 2019-20.
Mwenyekiti wake Bw Samuel Maina, amesema wataendelea kutumikia wanachama kwa uwazi na uwajibikaji licha ya kupitia changamoto tele katika mwaka uliopita wa 2019.
“Tunajua vyema ya kwamba tumepitia masaibu mengi ikiwemo mahasimu wetu kujaribu kutuhujumu. Hata hivyo, tutafanya juhudi kupiga hatua zaidi msimu huu,” alisema Bw Maina.
Kutokana na hamasisho kwa wanachama hao, wameshauriwa kujihusisha na shughuli zote zinazoendeshwa katika chama hicho na wasikubali kuyumbishwa kwa vyovyote vile.
Kulingana na chama hicho, tayari wamefanikiwa kutoa vyeti vya umiliki katika miradi 30 zilizoko chini yao na kwa hivyo wanachama walihimizwa kuwa na imani na chama chao.
“Tuko makini kuona ya kwamba tunakamilisha miradi yote iliyopangwa na kwa hivyo cha muhimu kwa sasa ni kuona ya kwamba wanachama wetu wanatuunga mkono kwa dhati,” alisema Bw Maina.
Alisema hali ya uchumi tayari imeweka mashirika mengi nchini katika hali ngumu jambo ambalo limelazimisha chama cha Urithi kuja na mbinu geni ya kujinasua kutoka katika masaibu hayo.
“Katika miezi michache ijayo tunajiweka katika hali ya kujinasua kutoka kwa hali ngumu ya kiuchumi na kuona ya kwamba tunapanga mikakati itakayotuweka mahali pazuri pa kujiendeleza kiuchumi,” alisema Bw Maina.
Alisema watatafuta ushirikiano kwa washika dau wengine ili kuweza kujiinua katika mikakati yao ya kibiashara.
Alisema chama hicho kitafanya juhudi kuona ya kwamba matakwa yote ya wanachama wake yanatimizwa kulingana na maoni yao.
Alisema wanafahamu vyema ya kwamba kuna watu fulani walio ndani ya chama hicho ambao wanajaribu kuwachochea watu kwa kuongea vibaya kuhusu chama hicho ili wanachama wagure, lakini walielezwa wawe macho.
Chama hicho kimetoa ushauri kwa kusema ya kwamba kila mwanachama ana haki ya kutoa malalamiko yake na wakati wowote wamehimizwa kupeleka malalamiko yao kwenye afisi kuu bila kuwa na woga wowote.