Wanachuo wanavyojikimu kimaisha wakati wa corona
NA HOSEA NAMACHANJA
Je, wanafunzi wa vyuo vikuu wanasukumaje gurudumu la maisha wakati huu wa janga la virusi vya corona kujikimu kimaisha?
Yajapo yapokee. Dunia inapoyumbishwa na ugonjwa wa corona, gharama ya maisha inashuhudiwa ikipanda kila kukicha huku baadhi ya kampuni zikiwafuta baadhi ya wafanyakazi na wanaosalia, mshahara wao ukipunguzwa.
Hapa nchini kwa upande mwingine, wanafunzi wa vyuo anuwai na vyuo vikuu kutoka sehemu tofauti kwa wakati huu, baadhi yao licha ya hali kuwa ngumu na wa kutegemewa siku za kesho, wameamua kutolaza damu na kufikiria mbinu mbadala za kusaka hela huku wakifuata sheria zilizowekwa na serikali za kuzuia maenezi ya maambukizi ya virusi vya corona.
Kevin Otenga, wa Chuo Kikuu cha Moi akiwa nyumbani Vihiga, tabia ya kuomba mzazi hasa akiwa nyumbani kama vile pesa za kununua kadihela na data za kuingia mtandao hapendi.
Jambo la kuomba usaidizi hulifanya akiwa shuleni kwa maana kule, hana nafasi ya kufanya kazi ya kupata pesa kando na masomo.
“Kwa wakati huu wa janga la virusi vya corona, ninamsaidia mzazi kazi ya kinu tulicho nacho nyumbani na mwisho wa siku, fedha nitakazokuwa nimezipata nitampa. Kando na hili, iwapo nitakuwa na uhitaji, nitamwomba na kunisaidia za kujikimu” asema.
Chepkemoi Sharon, wa Chuo Kikuu cha Chuka akiwa nyumbani Bomet, kulingana naye, bahati ni bidii na mtegemea cha mkoi, hanenepi mashavu.
“Mimi kila siku asubuhi huwa ninapika chai ya maziwa na mandazi kisha nawauzia watu wa karibu na soko la hapa kwetu. Wakati wa jioni, huwa siuzi kwa sababu ya kafyu,” asema.
Webukha Emmanuel Mabonga, wa Chuo Kikuu cha Moi akiwa Bungoma, kwake, njia pekee na nzuri zaidi ya kupata hela ni kilimo.
“Kusukuma gurudumu la maisha wakati huu wa ugonjwa wa corona, mimi huamka asubuhi na kuenda kupalilia matajiri mahindi yao vijijini na hela kidogo nizipatazo, ndizo huzitumia kujikimu kimaisha,” aliambia Taifa Leo Dijitali.
Hii ni ishara tosha kwamba licha ya kuwepo kwa corona, maisha lazima yasonge mbele kwani yasiposonga, atasonga mwenyewe.
Miriam Biketi, mwanachuo jijini Nairobi akiwa Webuye anasema hapendi hela za wavulana kutokana na uhusiano wa mapenzi maishani mwake.
“Mimi kama mwanafunzi, wakati huu mgumu wa janga la virusi vya corona, ninaishi bila hofu yoyote hasa upande wa hela. Nafanya upanzi wa mboga hasa za kienyeji kama vile managu, kunde, mrenda na dodo ambazo zinakua upesi. Mboga hizi ziwapo tayari, huziuza kwa wateja wangu ambao huja kondeni.
“Nina matunda kwa mfano ndizi, mapera na parachichi ambayo pia huuza na mwisho, nimewafuga kuku ambao hutaga mayai kisha yanapokuwa mengi huyauza,” anasema.
Wanafunzi hawa wanatumia kila mbinu wawezavyo kujikimu kimaisha namna wamejieleza. Wengine wakiwa wamekaa, wao wameona heri kuzumbua riziki kwa njia mbadala na kubalifu chambilecho, mwenye shoka hakosi kuni.