Habari Mseto

Wanafunzi wahama mabweni wakihofia shambulizi la kigaidi

June 5th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na NICHOLAS KOMU

WANAFUNZI wa tawi la Nyeri la Chuo cha Mafunzo ya Matibabu, wamehama mabweni kufuatia vitisho vya shambulio la kigaidi.

Baadhi ya wanafunzi wanaolala ndani ya chuo hicho kinachopatikana katika mtaa wa Kangemi mjini Nyeri, walihama kuanzia Jumamosi na kutafuta hifadhi kwa marafiki wanaolala nje ya chuo.

Polisi walitumwa katika chuo hicho wiki mbili zilizopita kufuatia madai kwamba magaidi walipanga kukishambulia.

Maafisa hao wamekuwa wakipiga doria chuoni na kuwahoji wanafunzi kuhusiana na vitisho hivyo.

Hospitali Kuu ya Nyeri inayopakana na chuo hicho pia imekuwa chini ya ulinzi mkali.

Wanafunzi walianza kuhama chuoni Jumamosi jioni baada ya habari kusambazwa miongoni mwao kwamba wangeshambuliwa. Habari hizo, kulingana na ripoti za polisi, zilianza katika bweni moja la wanafunzi wa kike.

“Tuligundua kwamba wanafunzi wa kike walikuwa wakihama bweni moja. Walituambia kwamba walikuwa wamepata ripoti kwamba chuo kingeshambuliwa,” alisema mwanafunzi mmoja ambaye aliomba tusitaje jina lake.

Ni wanafunzi 20 kutoka bweni hilo linaloishi wanafunzi 200 waliobaki chuoni huku wenzao wakihama.

Mkuu wa chuo hicho Bi Zipporah Njeru alisema wanafunzi hao waliripoti vitisho hivyo na polisi wakafahamishwa.

“Punde tu baada ya kupata habari hizo, tuliwafahamisha polisi na wakatuma maafisa kuimarisha ulinzi chuoni,” Bi Njeru alisema.

Wapelelezi waliotumwa chuoni Jumamosi waliwahoji baadhi ya wanafunzi na wafanyakazi kuhusiana na madai hayo.

Wanafunzi waliozungumza na Taifa Leo walisema wanalazimika kugawana gharama ya vyumba kwa hofu ya kushambuliwa wakirudi chuoni. Kiongozi wa wanafunzi Edison Mwendwa alisema kuna hofu na wengi wao hawajarudi chuoni.

“Bado tungali tumeshtuka. Wanafunzi wengi wangali wanaishi na wenzao nje ya chuo. Hatuhisi kuwa salama lakini tumefahamisha wasimamizi wa chuo,” alisema Bw Mwendwa.

Tukio la Jumamosi lilikuwa la pili katika muda wa wiki tatu la vitisho vya shambulio la kigaidi katika chuo hicho.

Ilisemekana kwamba shambulio la kwanza lilitoka kwa mwanabodaboda aliyefahamisha wanafunzi kwamba wangeshambuliwa.

Mkuu wa polisi eneo la Nyeri ya Kati, Muinde Kioko pia alisema wanafuatilia hali ilivyo na kuhakikishia wanafunzi kwamba tisho hilo limezimwa.

“Chuo hicho kiko salama na tunahakikishia wanafunzi kwamba tutawalinda. Hofu imekabiliwa na tunaendelea kutafuta habari hizo zilitoka wapi,” alisema.

Watu watatu wamekamatwa Nyeri kuhusiana na ugaidi na kukabidhiwa kitengo cha polisi wa kukabiliana na ugaidi (ATPU).