Habari Mseto

Wanafunzi wanaosomea udaktari washauriwa kurejea chuoni MKU Thika

September 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

CHUO Kikuu cha Mount Kenya (MKU) kimetoa ilani kwa wanafunzi wa mwaka wa mwisho wa masomo ya afya kuripoti chuoni Septemba 28, 2020.

Afisa mkuu wa usajili na usimamizi wa chuo hicho, Dkt Ronald G Maathai alisema uamuzi wa chuo ni kwamba wanafunzi wa kitengo cha afya wanastahili kujumuika na wahadhiri wao ana kwa ana ili kukamilisha masomo yaliyosalia.

“Baadhi ya wanafunzi wanaostahili kurejea ni wale wanaendesha masomo ya Bachelor of Science in Clinical Medicine, na Diploma in Clinical Medicine and Surgery. Wanafunzi hao pia wanastahili kuripoti kuanzia Septemba 28, 2020, hadi Oktoba 2, 2020.

Chuo hicho pia kimewaita chuoni wanafunzi wa somo la Digrii ya Somo kuhusu Dawa na Diploma ya Teknolojia ya Masuala ya Dawa.

Wanafunzi hao wote wanastahili kuwasiliana na wahadhiri wao ili kusoma ana kwa ana kwenye maabara.

“Masomo yao ni muhimu kwa sababu ni sharti mwanafunzi awe kwenye maabara na kuelezwa waziwazi mambo muhimu wanayostahili kujua,” alisema Dkt Maathai.

Hivi majuzi Waziri wa Elimu aliamuru wanafunzi wa mwaka wa mwisho chuoni warejee masomoni ili kuwasiliana na wahadhiri wao kupitia mitandaoni.

Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) pia imetoa ilani kwa walimu wa shule za msingi na za upili kuripoti katika shule zao kwa maandalizi ya wanafunzi kurejea masomoni.

“Tayari kamati inayoshughulika na mpango huo imekubaliana ya kwamba walimu wote warejee shuleni ili kufanya matayarisho ya mapema kabla ya wanafunzi kurejea rasmi,” alinukuliwa akisema hivi majuzi Bi Nancy Macharia afisa mkuu katika Tume ya kuajiri walimu (TSC).

Dkt Loice Odhiambo mkuu wa kitengo cha magonjwa ya maambukizi, Infectious Diseases Unit (IDU) katika hospitali ya Kenyatta alisema uchunguzi uliofanywa majuzi umebainisha kuwa homa ya corona imeshuka nchini na kiwango cha asilimia tano kwa muda wa wiki moja iliyopita.

Hata hivyo Wakenya bado wameshauriwa kufuata masharti yote yaliyowekwa na Wizara ya Afya ili kuzidi kupunguza kuenea kwa virusi hivyo.

Walimu pia watakuwa na kazi ya ziada watakaporejea shuleni kwa sababu watalazimika kuwahamasisha wanafunzi kila mara ili kukabiliana na Covid-19.

Wanafunzi na walimu pia watajipata katika mazingira tofauti kabisa wakirejea masomoni, baada ya mlipuko wa corona.