Wanafunzi wengi huabudu shetani nchini – Maaskofu
Na Titus Ominde
MAASKOFU wawili wamedai kuwa kuna ibada za shetani nchini hasa miongoni mwa wanafunzi.
Maskofu hao ambao ni askofu mkuu wa makanisa ya Aircan Divine Church John Chabuga na askofu mstaafu wa kanisa la Kiangilikana dayosisi ya Eldoret Thomas Kogo.
Kwa mujibu wa maskofu hao, ongezeko la kuabudu shetani miongoni mwa wanafunzi ni tishio kwa maadili mema siku za usoni. Askofu Chabuga alitaka serikali itafute mbinu bora ya kutatatua tatizo hilo kwa ushirikiano na viongozi wa kidini ili kulinda hatima ya nchi.
Askofu Chabuga alisema viwango vya uabudu shetani miongoni mwa vijana vimeogezeka kutokana na kutowajibika kwa wazazi.
“Wazazi wanapaswa kuwajibikia majukumu yao ya kuona kuwa watoto wao wanashiriki ibada ya kweli. Baadhi ya wazazi hawajali kuhusu masuala ya imani ya watoto hao na tabia hii ni hatari kwa imani ya watoto wetu,” alisema askofu Chabuga.
Naye askofu Kogo alitahadharisha walimu dhidi ya kufukuza shuleni watoto ambao hushukiwa kuwa waabudu shetani badala yake watoto kama hao wanapaswa kupewa ushauri nasaha na kuombewa na wahubiri wa kweli.
Askofu Kogo alihusisha ajali nyingi ambazo zinatokea humu nchini na ibada ya mashetani, huku akitaka serikali kuingilia kati na kubuni mbinu ya kukabiliana na tatizo hilo.
Askofu huyo alidai kuwa baadhi ya vijana ambao huabudu mashetani hasajiliwa kujiunga na makundi ya kigaidi kama vile Al shaabab.