• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 AM
Wanahabari wakataa tuzo za Wizara ya Kawi

Wanahabari wakataa tuzo za Wizara ya Kawi

PETER MBURU na ANTHONY KITIMO

WIZARA za Mafuta na Kawi zililazimika kufutilia mbali hafla ya kutuza wanahabari, iliyokuwa imepangwa jijini Nairobi leo, baada ya miungano ya wanahabari na wahariri kukataa mwaliko.

Katibu wa wizara ya Mafuta Andrew Kamau alisema walichukua hatua hiyo kwa ushauri kutoka kwa Baraza la Kusimamia Vyombo vya Habari Kenya (MCK), saa kadhaa baada ya Muungano wa Wanahabari Nchini (KUJ) na ule wa Wahariri (Editors’ Guild) kusema wasingeshiriki.

Miungano hiyo ilitaja hafla hiyo kuwa inayoweza kukwaza uhuru wa uanahabari Kenya. Iliilaumu kampuni ya Kenya Pipeline (KPC) kuwa isiyo na maadili imara ya kuwa katika nafasi ya kuwatuza wanahabari.

KPC ilikuwa imealika wanahabari pamoja na miungano hiyo kwa tuzo za EJEA awamu ya 2019 ambazo zingefanywa Alhamisi katika hoteli ya Safari Park.

“Baraza Kuu la Muungano wa Wahariri limeonelea kuwa tuzo za EJEA kwa sasa zinaweza kuonekana kama kikwazo kwa uhuru katika uanahabari nchini Kenya,” barua kutoka kwa Afisa Mkuu Mtendaji wa muungano huo Rosalia Omungo mnamo Aprili 1 ilisema.

Barua kutoka kwa Katibu Mkuu wa KUJ, Bw Erick Oduor nayo ilisema kuwa kampuni ya KPC imeshirikiana na kampuni ambazo zinachunguzwa kuhusu madai ya ufisadi kuandaa hafla hiyo, na hivyo haikuwa na msingi wa kimaadili.

“Tunataka kujitenga na tuzo hizo kwani tunaamini kuwa hazizingatii maadili. Tunafahamu kuwa baadhi ya kampuni ambazo zimefadhili hafla hiyo ama zimechunguzwa au zinachunguzwa kuhusu madai ya ufisadi na hivyo haziwezi kuwa na maadili ambayo kama wanahabari tunajihusisha nayo,” akasema Bw Oduor.

Baada ya ujumbe wa miungano hiyo, Bw Kamau alisema “Ukimkaribisha mgeni kwa mlo nyumbani kwako na akwambie hatakuja unaendelea na mpango huo kweli?”

Afisa huyo alisema wazo hilo lilikuwa la wanahabari mwanzoni, ambao walionyesha ari ya kutaka kufahamu zaidi kuhusu masuala ya kawi.

Afisa Mkuu Mtendaji wa MCK David Omwoyo pia alisema hatua ya kufutilia mbali hafla hiyo inalenga kutoa nafasi kwa mashauriano.

Bw Omwoyo alisema kuwa japo ni vyema kwa wizara hizo kuwekeza kwenye vyombo vya habari, hilo linafaa kufanywa kwa umakini ili isionekane kama hatua hiyo inakwaza uhuru wa uanahabari.

“MCK imeshauriana na Wizara ya Mafuta na kushauri kuwa hafla hiyo isitishwe. Washikadau katika sekta ya uanahabari hawajaridhishwa na tuzo haswa ufadhili wa kifedha, wakati ambapo uhuru wa wanahabari ambao kimaadili hawawezi kutuzwa na watu/mashirika ambayo yanaripoti kuyahusu,” Bw Omwoyo akasema.

Dhuluma za kimapenzi

Kwengineko mjini Mombasa, idara ya watoto imeboresha mikakati yake ya kupambana na visa vya unyanyasaji watoto kingono wakati huu wa likizo.

Afisa mkuu wa watoto kaunti hiyo , Bw Philip Nzenge, alisema wameanza kutumia njia za kisasa za kueneza ujumbe kukabiliana na visa hivyo ili kufikia idadi kubwa ya watu kwa muda mfupi.

Visa vingi vya watoto kunyanyaswa kingono vimekuwa vikiripotiwa wakati wa likizo, jambo ambalo limewafanya kuchukua mikakati hiyo ili kukomesha tabia hiyo.

“Tumeandaa jumbe mbalimbali ambazo zinawalenga wakazi na watalii ambao huzuru mji huu wakati wa likizo. Tutatumia teknolojia ili kufikisha jumbe hizo kama onyo kwa wanaoeneza visa hivyo,” alisema Bw Nzenge.

You can share this post!

Washukiwa wa MRC wazuiliwa kwa siku 14

Mawakala bondeni wapunja wakuzaji mahindi mamilioni

adminleo