Habari Mseto

Wanaharakati na viongozi Mombasa wapinga agizo kontena zote zisafirishwe kwa SGR

June 10th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na WINNIE ATIENO

BAADHI ya viongozi wa Kaunti ya Mombasa na wanaharakati wamepinga agizo la serikali kwamba kontena zote kutoka bandari ya Mombasa zisafirishwe kwa treni zinazotumia reli ya kisasa SGR hadi Suswa huko Naivasha.

Wadau hao kutoka sekta ya uchukuzi wamepinga hatua hiyo wakisisitiza kuwa itaua na kuathiri uchumi wa Pwani.

Viongozi hao wakiongozwa na Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir wamesema Jumatano wenye kontena wanafaa kuwa na uhuru na hiari ya kuchagua ama SGR au malori.

Madereva wa masafa marefu wamekuwa wakiishtumu serikali kwa hatua hiyo wakisema watakosa ajira.

“Si leo tu lakini nimekuwa katika mstari wa mbele kuhakikisha uchumi wetu sisi na miji yote ikiwemo Naivasha inastawika. Hatuwezi kusema ghalfa kwamba kontena zote zibebwe kwa treni za SGR. Uchumi wetu tayari uko chini na hatuwezi kukubali,” alisema Bw Nassir.

Bw Nassir amesema serikali haifai kuweka vikwazo katika sekta hiyo.

Nao muungano wa madereva unadai kuwa serikali ina mpango wa kusafirisha mizigo yote kutoka bandarini kupitia reli ya SGR na kuwanyima biashara, mapato na hata ajira.

“Si sawa kwa reli ya SGR kupewa kipaumbele; serikali inafaa kutuelezea bayana kama ni swala la deni la SGR basi liwekwe wazi,” alisema mkurugenzi mkuu wa muungano huo Bw Dennis Ombok.