Habari Mseto

Wanajeshi sasa lawamani kwa kutookoa wavuvi

December 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na WACHIRA MWANGI

WAVUVI wanne kutoka Kaunti ya Tana River wamelaumu maafisa wa jeshi la wanamaji kwa kukataa kuwaokoa walipokwama baharini kwa zaidi ya wiki mbili.

MaBw Malik Mbwana, Edward Munga, Baraka Kahindi Thoya na Juma Samuel Nzai ambao wanatoka eneo la Kipini, walikuwa wameenda kuvua samaki katika Bahari Hindi mnamo Desemba 9, 2019, mawimbi yalipoanza kuwatatiza.

Mawimbi makali yaliyoandamana na mvua kubwa yalilazimisha boti yao kusukumwa hadi sehemu ya bahari yenye kina kirefu ambako walihangaika kwa siku 17.

“Tulikuwa tumeenda baharini kama kawaida kuendesha shughuli zetu za uvuvi tulipokumbana na mawimbi makali na mvua kubwa iliyotusukuma hadi katikati ya bahari. Hatimaye tuliishiwa na mafuta na tukashindwa kupata dira kuhusu tulikokuwa,” akasema Bw Mbwana ambaye ndiye alikuwa nahodha wa boti hiyo.

“Asubuhi iliyofuata, tulijipata hatuna chakula na maji na hatukujua la kufanya,” akaeleza baada ya wao kuokolewa majira ya alfajiri siku ya Krismasi.

Bw Mbwana alisema awali waliona boti ya jeshi la wanamaji ikiwa na maafisa wanane wakishika doria, wakawaona lakini hawakufanya lolote kuwasaidia.

“Lakini tulivunjika moyo tulipoona boti ikienda bila kutusaidia kama tulivyotarajia. Tuliwaomba watusaidie hata kwa maji na chakula kwani mmoja wetu alikuwa akiugua, lakini walipuuza maombi yetu na kwenda zao,” akaeleza.

Kitendo cha wanajeshi hao kililaaniwa vikali na wananchi huku Wakenya kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter wakikitaja kama cha kusikitisha.

Jaribio letu kupata maelezo kutoka kwa jeshi la wanamaji halikufua dafu kwani afisi yao ya mawasiliano haikuwa imejibu maswali yetu kufikia wakati wa kwenda mitamboni.

Mbwana, 37, ambaye amehudumu kama nahodha wa boti hiyo, kwa jina Yahafidh, alisema asingetaka mtu mwingine kupitia masaibu waliyokumbana nayo katika muda huo wa majuma mawili.

“Siku ya nane tulipata bahati kwa sababu mvua ilinyesha. Tukatumia ndoo kuteka maji ya mvua ili kunywa.”

Nyumbani, jamaa zao walijawa na huzuni kuu baada ya wavuvi hao wanne kupotea baharini. Walipokosa kurejea familia zilipiga ripoti katika kituo cha polisi cha Kipini, nambari OB 09/10/12/2019.

Msako

Kaka mkubwa wa Munga, John Mramba, alisema polisi na wakazi walifanya msako lakini hawakufaulu.

“Polisi wa bahari walijiunga na msako huo ulioendeshwa hadi Mombasa, lakini hawakuwapata,” akaambia Taifa Leo.

“Ilidhaniwa kuwa wanne hao walikuwa wamekufa. Hata hivyo, tulivumilia hali mbaya ya anga huku tukiwa na matumaini kuwa wangepatikana,” akasema Bw Mramba.

Mbwana alisema walivumilia hali ngumu ya anga lakini bado walikuwa na matumaini kwamba wangepata usaidizi.

Waliendelea kuelea baharini siku hizo zote. Siku ya Krismasi mwendo wa saa tisa mchana, chombo chao kilisonga karibu na kijiji cha Ngomeni, Kaunti ya Kilifi, umbali wa kilomita 27 kutoka mji wa Malindi.

“Kwa kuwa hatukuwa na mafuta tunaamini ni Mungu tu alituwezesha kurejea karibu na ufuo na tukarejea manyumbani mwetu baada ya kukaa baharini mwa siku 17,” Bw Mbwana akasema.