Wanamageuzi wataka Katiba ya 2010 itekelezwe kikamilifu
Na BENSON MATHEKA
WANAHARAKATI nchini wanataka Katiba ya 2010 itekelezwe kwa kikamilifu huku wakipinga mabadiliko ambayo yatalenga kuwafaidi wachache.
Wanaharakati hao walitoa maoni yao wakiwa katika maeneo tofauti wakati wa maadhimisho ya mwaka wa 30 wa siku ya Saba Saba ambayo wapiganiaji wa demokrasia ya vyama vingi walitumia kuandamana kushinikiza serikali kukubali mabadiliko.
Ingawa maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika kukiwa na juhudi za kubadilisha katiba, wanaharakati wanasema kwamba mchakato huo hautakuwa na maana iwapo haunuii kufaidi mwananchi wa kawaida.
Wanasema kwamba katiba iliyopitishwa 2010 inafaa kutekelezwa kikamilifu hasa kifungu cha sita kuhusu maadili na utawala.
Kulingana na aliyekuwa mbunge wa Subukia, Bw Koigi Wa Wamwere, katiba haifai kubadilishwa ili kufaidi wachache hasa familia zenye ushawishi.
“Mchakato wa kubadilisha katiba unaolenga kufaidi wananchi wote unakubalika. Ndilo lilikuwa lengo la wapiganiaji wa katiba mpya waliomwaga damu yao kukomboa Wakenya. Kubadilisha katiba ili kutimiza maslahi ya wachache wenye ushawishi au ya muda mfupi ni hatari,” akasema Bw Wamwere.
Kasisi mstaafu wa kanisa la PCEA, Bw Timothy Njoya ambaye alikuwa mstari wa mbele kupigania demokrasia ya vyama vingi anataja mchakato unaoendelea wa kubadilisha katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI) kama ufufuko wa shetani akisema kuna watu wanaotaka kuutumia kukandamiza maskini.
“BBI ni kurudisha maovu, kutumia utamaduni na dini na kufanya Nairobi kuwa hekalu ambalo kwa kisingizio cha handisheki, mapapa matajiri watatafuna Wakenya milele,” akasema Kasisi Njoya.
Kiongozi wa chama cha Narc Kenya Martha Karua alikumbuka kwamba wakati wa maandamano ya Saba Saba wanasheria walikuwa kwenye mstari wa mbele kupigania mabadiliko.
“Chama cha Wanasheria kilikuwa mstari wa mbele, mawakili walisusia mahakama kwa siku 21, hadi viongozi wao waliokamatwa wakaachiliwa. Walikuwa wakitetea wanaharakati waliokamatwa kwa kuongoza na kushiriki maandamano bila malipo.”
Wanaharakati wanasema kwamba miaka kumi baada ya katiba mpya kupitishwa, haijatekelezwa kikamilifu huku haki za Wakenya maskini zikiendelea kukiukwa.
“Wakenya wana haki ya kujikomboa kutokana na njaa. Katiba yetu inasema ni haki ya kila Mkenya kupata chakula bora na salama. Badala ya kutekeleza hitaji hili, kuna miito ya kuibadilisha,” alisema mwanaharakati Bonny Orengo.
Alisema ingawa katiba inahakikishia Wakenya wa matabaka usalama wao, mauaji ya kiholela yanaendelea.
“Wakenya wako na safari ndefu ya kujikomboa. Sio kwamba hawana katiba, ni walio mamlakani ambao hawataki kuitekeleza ili waendelee kukandamiza maskini kwa kutumia polisi kuua vijana,” alisema mwanaharakati Gathangu Ndungu.
Mashirika kadhaa ya kutetea haki za binadamu yanapanga maandamano ya amani jijini Nairobi kuadhimisha siku ya Saba Saba mwaka huu wakisema haifai kufifia.