Wanaoishi karibu na bwawa la Kiambere kupata umeme na maji
Na MWANGI MUIRURI
SERIKALI sasa imekubali kutoa miradi ya maji na umeme kwa wakazi wanaoishi karibu na bwawa la uzalishaji kawi la Kiambere lililoko katika Kaunti ya Embu.
Hatua hii imeafikiwa baada ya wakazi hao kusukuma asasi za kiserikali kwa muda sasa wakiteta kuwa licha ya kuwa karibu na bwawa hilo, wao wamekuwa wakiishi bila maji safi na umeme.
Katika ujumbe wa Jumatatu kutoka afisi ya Gavana kwa wawakilishi wa jamii zinazoishi karibu na bwawa hilo, serikali kuu sasa itatimiza asilimia 100 ya mapendekezo yao kabla ya Juni 2020.
Wenyeji hao wamekuwa wakiandamana, kuandika barua za malalamiko na pia kuwashinikiza viongozi wao wakiitaka serikali kuwaahidi miradi hiyo kwa haraka.
Waliteta kuwa Embu ina mabwawa matano ya kuzalisha umeme na ambayo hutoa asilimia 60 ya nguvu za umeme kitaifa lakini wao wamekuwa wakiishi kwa giza na bila huduma ya maji safi.
Chakula cha mamba
Waliteta kuwa wao wametengwa kimaendeleo na kuwa wamefanywa chakula cha mamba ambao mara kwa mara huwashambulia na kuwaua.
Januari 26, 2019, Bi Joyce Ruguru aliuawa na mamba alipokuwa akiteka maji ya bwawa hilo.
Kwa wakati mmoja, wakazi hao walitishia kusambaratisha mtambo unaotoa umeme kutoka Kiambere na Kindaruma hadi Kamburu ikiwa matakwa yao hayangetimizwa.
Ilibidi maafisa wa usalama wakiongozwa na Mkuu wa Polisi wa Mbeere Bw Tom Odera na Mkuu wa Wilaya Bw Abdi Khalif kujitokeza ili kuwazuia kutekeleza kitisho hicho.
Hata hivyo, lau wangejaribu kutekeleza kitisho hilo, wangekuwa wanajiingiza kwenye hatari kwani nyaya hizo husambaza nguvu nyingi sana za umeme na hivyo kuwa hatari kwa maisha yao.
Afisa wa Shirika la KPLC Bw John Gachuri aliambia Taifa Leo kuwa wakazi wa Mutuovare wataunganishwa na huduma za umeme kabla ya Julai kuisha na kuwa tayari shughuli za usoroveya zimeanza.
Kwa upande wake, afisa wa huduma za maji Bw Phillip Kabiru alisema serikali itaanzisha usambazaji wa maji kuanzia eneo la Kirie hadi Mutuovare.
Diwani wa Kiambere Bw Francis Njuki alisema wakazi wametulia kwa sasa wakingoja kuona kama serikali itatimiza ahadi hizo kwa wakati unaofaa na ikiwa ni hadaa, huenda wakafanya maandamano ya kusaka haki dhidi ya serikali.