Wanaompinga Kinoti wanahofia kukamatwa -Wabunge
Na PETER MBURU
HAKUNA mtu anaweza kuikosoa Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) ikiwa hakuna kosa amefanya, Kamati ya Bunge kuhusu Usalama sasa imesema.
Kamati hiyo imewakashifu viongozi ambao wamekuwa wakiivamia idara ya DCI kuwa inaendesha vita dhidi ya ufisadi kwa mapendeleo na kuwalenga watu fulani, ikisema wanajua wanachoficha.
Wanachama wa kamati hiyo wamesema wataiunga mkono idara hiyo kuendeleza kazi yake namna imekuwa ikifanya, wakiahidi hata kupigania kurekebishwa kwa sheria ili ipewe nguvu zaidi za kufanya maamuzi na kuongezewa bajeti.
Wabunge hao walikuwa wamezuru Makao Makuu ya DCI kwenye barabara ya Kiambu kukagua maabara ya kisasa ambayo itatumika kufanyia uchunguzi wa makosa ya jinai na ambayo itafanya Kenya kuacha kutegemea nchi zingine kwa uchunguzi wa baadhi ya makosa hatari Alhamisi.
“Vita ambavyo vinaendelea nchini vitaendelea kuendeshwa hivi bila kumpendelea yeyote kwani katiba inasema hivyo. Labda kama unahofia kwa kuwa umefanya kitu, hufai kuogopa DCI.
“Tumezungumza na viongozi wa idara mbalimbali na naweza kusema bila wasiwasi kuwa hakuna mtu anafaa kuogopa DCI kuwa atasingiziwa makosa, ikiwa hujakosea, mbona uogope?” mwenyekiti wa kamati hiyo Paul Koinange akasema.
Bw Koinange, ambaye pia ni mbunge wa Kiambaa aliahidi kuwa wabunge watapigania idara ya DCI iongezewe pesa kutokana na kazi ambayo inafanya, ambapo wakati mwingine wanasafiri nje ya nchi kwenda kufanya uchunguzi.
“Tutawaunga mkono hata katika masuala ya sheria ili waweze kufanya kazi kwa nguvu na kufanya maamuzi katika kesi tofauti wakijiamini,” akasema Bw Koinange.
“Tutawaunga mkono kwenye suala la bajeti, sharti tuongeze pesa zinazopewa idara hii kwani wakati mwingine wanasafiri nje ya nchi kufanya uchunguzi, haya masuala si ya Kenya pekee, Kenya ni sehemu ya jamii ya dunia. Watu wanatoka nje kufanya biashara humu nasi tunasafiri kwenda kufanya uchunguzi,” akasema.
Bw Kinoti alisema kuwa maabara hiyo mpya itakuwa na idara saba ambazo huduma zake hazipatikani nchini na ambazo zimekuwa zikilazimu Kenya kutegemea mataifa mengine, kama uchunguzi wa DNA na hivyo kuchelewesha uchunguzi.
“Sasa tumebadilisha baadhi ya vifaa na kuleta vingine vyenye ubora wa hali ya juu, mbali na kuongeza idara saba ambazo hatukuwa nazo,” akasema Bw Kinoti.
Idara ya DCI inasema kuwa kwa sasa inachunguza takriban kesi 60 zenye uzito mkubwa, kati ya nyingine nyingi, ikisema kuwa inataka kukamilisha uchunguzi na kupata ushahidi wa kina na wa kutosha, kabla ya kuzishtaki kortini.
Bw Kinoti aidha alisema idara yake itakuwa ikishirikiana na wapasuaji wa maiti wa serikali katika uchunguzi wa vifo vinavyohusishwa na jinai, ili kuzuia visa ambapo inahofiwa kuwa ripoti zao zimekorogwa, kama jinsi imekuwa ikifanyika mbeleni.
Wabunge waliilaumu Idara ya Mahakama kuwa imekuwa ikivuta nyuma juhudi za DCI kwa kuchelewesha kesi kortini, wakiiomba kushirikiana na wachunguzi ili kesi ziharakishwe kusikizwa na kuamuliwa.
“Hiyo ndiyo shida kubwa sana tuliyo nayo nchini,” akasema Bw Kinoti.