Habari Mseto

Wanaouza mafuta yenye rangi waonywa na KEBS

October 23rd, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na BERNARDINE MUTANU

Shirika la Kukadiria Ubora wa Bidhaa nchini (KEBS) limeonya waagizaji wa mafuta yanayochanganywa na rangi, mafuta ya kulainisha, na mafuta yaliyotumika dhidi ya kwenda kinyume na viwango vilivyowekwa kwa bidhaa hizo kuagizwa nchini.

KEBS ilisema ilikuwa na habari kwamba waagizaji wa bidhaa hizo wanafanya hivyo bila kuambatisha uchunguzi wa mahabara.

Kulingana na shirika hilo, lazima bidhaa hizo zichunguzwe, kukaguliwa na kuwa na cheti cha kuthibitisha kwamba uagizaji wake unafuata kanuni na ripoti ya uchunguzi ili ziweze kuruhusiwa kupita forodhani.

Katika taarifa Jumanne, shirika hilo lilisema ripoti zote kuhusiana na bidhaa hizo zitaidhinishwa, kuchukuliwa sampuli na kuachiliwa zikipatikana kutimiza matakwa yote.

“Tumepata kufahamu kwamba sio kampuni zote za bidhaa hizo zinafuata kanuni,” alisema kaimu mkurugenzi Moses Ikiara.

Hii ni baada ya Shirika la Kusimamia Mazingira (NEMA) kuelezea hofu yake kwamba baadhi ya bidhaa zinazoagizwa nchini ni za ubora wa chini sana.