Habari Mseto

Wanasiasa lawamani kwa zogo la ngamia

September 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na KITAVI MUTUA

WAKAZI wa Mutha, Kitui Kusini, Kaunti ya Kitui, wamewashutumu polisi kwa kushindwa kuwafukuza maelfu ya ngamia wanaovamia mashamba yao, wakidai wanyama hao wanamilikiwa na watu mashuhuri serikalini.

Visa hivyo vya uvamizi wa maelfu ya ngamia kila mwaka vimeibua madai kwamba polisi wametiwa ‘mifukoni’ na watu hao mashuhuri, ili wasiwaondoe wanyama hao ambao husababisha uharibifu mkubwa.

Wakazi wanadai kuwa wanapoenda kupiga ripoti katika kituo cha Mutha, wanaulizwa maswali magumu kabla ya kuandikisha taarifa zao.

“Maswali ambayo polisi wanauliza yamewaacha wakazi vinywa wazi. Wanashangaa kwa nini wanatakiwa kujua alama spesheli za utambuzi wa ngamia hao, kama si kwamba polisi wanawafahamu wamiliki,” akasema diwani wa zamani wa hapo Bw Allan Kavindi, ambaye ana duka katika soko la Mutha.

Inasemekana watu fulani mashuhuri kutoka Kaskazini Mashariki –wakiwemo wabunge wawili maarufu, jaji ambaye amehudumu kwa miaka mingi na gavana mmoja wa sasa – huzuru Mutha mara kwa mara kukagua mifugo yao.

Madai hayo yalizidi baada ya mbunge wa hapo Dkt Racheal Nyamai kutishia kufichua majina ya watu mashuhuri serikalini, ambao aliwashutumu kwa kuwalinda wavamizi wanaohangaisha wakazi wa eneo-bunge lake.

Manufaa

Dkt Nyamai (Jubilee) alidai kuwa mzozo usiokoma baina ya jamii za Kitui na wafugaji kutoka kaunti za Kaskazini Mashariki, unachochewa na maafisa fulani wa ngazi za juu serikalini kwa manufaa yao ya kibinafsi.

Lakini Naibu Kamishna wa Kauntindogo ya Mutomo, Bw Ronald Enyakasi, alisema serikali inachukulia mzozo huo kama wa kawaida baina ya wakulima na wafugaji wanaosaka malisho na maji kwa mifugo wao.

Hata hivyo, Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai alipozuru eneo hilo Ijumaa, alishuhudia hali halisi baada ya ujumbe wake kukumbana ana kwa ana na makundi kadhaa ya zaidi ya ngamia elfu nne kila moja.

Bw Mutyambai ambaye alikuwa ameandamana na Mkurugenzi wa Idara ya Uchunuguzi wa Jinai, Bw George Kinoti, na Mkurugenzi wa Ofisi ya Mashtaka ya Umma, Bw Noordin Haji, alisema uchunguzi umeanzishwa kubaini wamiliki wa ngamia hao.