Wanawake walioandamana wapata mabadiliko ya mzunguko wa hedhi
MABADILIKO ya mzunguko wa hedhi miongoni mwa wanawake na wasichana yameshuhudiwa kwa baadhi ya wale waliondamana siku ya Jumanne, wiki iliyopita.
Kwenye mtandao wa X, wengi walilalamikia mabadiliko hayo.
“Wacha nikuambie, siku ya Jumanne, nilikuwa mgonjwa. Baada ya kufika nyumbani nilianza kutokwa na damu. Kumbe ni kwa sababu ya kemikali za vitoa machozi,” alisema mtumiaji wa X.
Kulingana na wataalamu, mabadiliko yasiyokuwa ya kawaida kwa hedhi za wanawake yalichangiwa na gesi ya vitoa machozi ambayo husababisha athari za kisaikolojia na mzunguko wa hedhi.
Gesi ya kutoa machozi huwa na mchanganyiko wa kemikali zinazojulikana kuathari mfumo wa upumuaji, ngozi, na macho. Hata hivyo, athari zake kwa afya ya uzazi, ikiwa ni pamoja na mzunguko wa hedhi, pia imekuwa suala la wasiwasi.
Daktari wa Uzazi katika hospitali ya Aga Khan, Bw Dennis Miskellah, alisema matukio hayo yanahusishwa na vipindi vya mfadhaiko.
Dkt Miskellah alisisitiza kwamba matukio kama vile maandamano, ambayo asili yake yana mfadhaiko kwa wanawake yanaweza pia kusababisha mabadiliko hayo.
“Miili yetu hufanya kazi kupitia mwingiliano wa kemikali unaoendeshwa na homoni. Homoni hizi sio tu huathiri mzunguko wa hedhi lakini pia huathiri hisia zetu. Uchunguzi umeonyesha kuwa mkazo unaweza kubadilisha kwa kiasi kikubwa mfumo wa hedhi wa mwanamke,” alieleza Dkt Miskellah.