• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Wandani wa Ruto waapa kuupinga mswada wa jinsia

Wandani wa Ruto waapa kuupinga mswada wa jinsia

PETER MBURU na SHABAN MAKOKHA

KIKUNDI cha wabunge wa Jubilee wamekaidi wito wa naibu wa Rais William Ruto kuwa wauunge mkono mswada wa kiongozi wa wengi bungeni Aden Duale wa kutaka idadi ya wabunge wa kike iongezwe.

Bw Duale anapendekeza kuwa ili kuwa na usawa wa jinsia katika uwakilishi bungeni, katiba ifanyiwe marekebisho ili idadi ya wabunge wanawake iongezwe, suala litakalosababisha kuongezeka kwa idadi jumla ya viongozi hao kutoka 349 hadi 391 katika bunge la taifa na 67 hadi 71 seneti.

Mswada wa Bw Duale unapendekeza kuwe na uteuzi spesheli wa wanawake kulingana na umaarufu wa chama katika bunge kila baada ya uchaguzi ili usawa wa jinsia uafikiwe.

Hata hivyo, pendekezo la kiongozi huyu limekosolewa kuwa linalenga kuongeza kiwango cha matumizi ya pesa za umma kwa mishahara, wakati ambapo taifa linataka kurekebisha Katiba ili kupunguza gharama ya matumizi.

Jumamosi, Bw Ruto aliwashawishi wabunge kuunga mkono, baada ya pingamizi kuibuka kuuhusu ndani ya Jubilee.

“Wanawake wetu ambao wanajumuisha asilimia 50 ya idadi ya watu wanahitaji fursa ya kuhusishwa katika uongozi wa taifa letu. Ninatumai kuwa mambo yatakuwa mazuri wakati huu,” Bw Ruto alisema.

Hata hivyo, baadhi ya wabunge ambao ni wandani wake na wengine kutoka ngome yake ya Bonde la Ufa walipinga ombi hilo, wakisema wataupinga mswada wa Bw Duale.

Wabunge Alfred Keter wa Nandi Hills, Joshua Kuttuny wa Cherangany na Silas Tiren wa Moiben walieleza kuwa wanachotaka ni wakulima wa eneo hilo kutatuliwa matatizo katika sekta ya kilimo, badala ya kuambiwa kuhusu usawa wa jinsia bungeni.

“Rekebisheni mambo ya mahindi na mbolea kwanza. Mambo ya kutishwa hapa hatutaki,” Bw Keter akasema.

Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria naye kwenye akaunti yake ya Facebook alichapisha sababu zitakazomfanya kuupinga mswada huo utakapofikishwa bungeni kesho.

“Sheria ya usawa wa jinsia ilinuiwa kuhamasisha taifa kuchangamkia suala hilo wala si kuunda kipengee cha Katiba. Jumanne nitaupinga mswada huo kwa kuwa utaongeza wabunge 56 wakati taifa liko katika zoezi la Punguza Mzigo,” akasema Bw Kuria.

Hata hivyo, baadhi ya viongozi wameahidi kuuunga mkono mswada huo kama njia ya kutetea nafasi ya wanawake uongozini.

Wawakilishi wanawake Catherine Waruguru (Laikipia), Amina Gedo (Mandera), Joyce Kameme (Machakos), Purity Wangui (Kirinyaga), Faith Gitau (Nyandarua), Irene Kasalu (Kitui), Beatrice Adagala (Vihiga) na Elsie Muhanda (Kakamega) Jumamosi walipigia debe mswada huo, wakisema utaleta usawa uongozini.

Wabunge Godfrey Osotsi, Benjamin Washiali, Didmus Baraza, Malulu Injendi, Mwambu Mabonga, Emmanuel Wangwe na Bernard Shinali nao aidha waliahidi kuunga mkono mswada huo.

Mswada huo wa Bw Duale vilevile umekosolewa na wataalamu wa kisheria kuwa ulio na pengo kwa kuwa huenda ukahitaji sheria hiyo kubadilishwa kila wakati wa uchaguzi kwa kuwa idadi ya jinsia itakayochaguliwa haiwezikubashirika kabla ya uchaguzi kufanyika.

You can share this post!

LSK kuchunguza kiini cha nusu ya wanasheria kufeli mtihani

KCSE: Mtahiniwa afariki baada ya kugongwa tumboni

adminleo