• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
Wandani wa Ruto wataka Raila astaafu na Uhuru

Wandani wa Ruto wataka Raila astaafu na Uhuru

NA PIUS MAUNDU

WANDANI wa Naibu Rais Dkt William Ruto sasa wanamtaka Kinara wa ODM Raila Odinga astaafu siasa pamoja na Rais Uhuru Kenyatta ifikapo uchaguzi wa 2022.

Wabunge Aisha Jumwa(Malindi), Moses Kuria(Gatundu Kusini) na Vincent Musyoka(Mwala) pia walisema juhudi zinazoendelezwa na Rais na Bw Odinga hazitaunganisha taifa hili kamwe.

Wanasiasa hao walishikilia kwamba kutekelezwa kwa mapendekezo kwenye ripoti ya Jopokazi la Maridhiano(BBI) iliyotolewa hivi majuzi, hakutamaliza ghasia baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa.

Ripoti hiyo tayari imekabidhiwa Rais Kenyatta na Bw Odinga ambao waliingia kwenye ndoa ya kisiasa mnamo mwezi Machi mwaka uliopita.

“Ripoti ya BBI haitaunganisha nchi hii. Njia pekee ya kuunganisha taifa hili na kuhakikisha amani inadumu na kwa Bw Odinga kujiondoa kwenye siasa na kustaafu pamoja na Rais Uhuru Kenyatta mnamo 2022,” akasema Bw Kuria ambaye pia ni mbunge nyumbani kwa Rais kaunti ya Kiambu.

Wabunge hao walikuwa wakizungumza jana katika kanisa Katoliki la Mukuyuni wakati wa mchango wa kusaidia kanisa hilo kumaliza jengo lake ambapo waliandamana na Dkt Ruto.

Naibu Rais alitoa mchango wa kibinafsi wa Sh1.5 milioni na kuunga kauli ya wabunge hao kuhusu jitihada za kuhakikisha taifa hili linaunganishwa na ghasia za baada ya uchaguzi zinatokomezwa milele.

“Sisi tunatilia manani kutekelezwa kwa mageuzi nchini. Njia pekee ya kuafikia hilo ni kuwaleta Wakenya pamoja na kutatua masuala yanayowaathiri kimaendeleo. Taifa haliwezi kusonga mbele kupitia sarakasi za kila mara,” akasema Dkt Ruto.

Naibu Gavana wa Makueni Adelina Mwau aliwataka wabunge na kanisa kuwasaidia raia kuelewa kwa mapana na marefu yaliyomo ndani ya ripoti ya BBI na kuwaomba wanasiasa kushiriki mjadala ambao unaunganisha taifa badala ya kuligawanya kuhusu ripoti hiyo.

Kwa upande wake, Bw Musyoka alishikilia kwamba wataendelea kumuunga mkono Naibu Rais na hawapingi kivyovyote ripoti ya BBI.

“Sisi tumeamua kufuata mwelekeo wowote kwenye BBI. Jambo zuri ni kwamba ripoti hiyo haipendekezi kubuniwa kwa vyeo kadhaa ili kuwatunuku wanasiasa nyadhifa mbalimbali,

“Wale wanaovumisha BBI wanafaa kupigania mamlaka zaidi yatolewe kwa kiongozi wa upinzani kwa sababu watahitaji kiti hicho baada ya uchaguzi mkuu,” akasema Bw Musyoka.

Mbunge huyo wa chama cha MCC ambaye anahudumu muhula wake wa pili alieleza kusikitishwa kwake na hali ya sasa ya kisiasa, akimlaumu Bw Odinga kwa kufaulu kuvuruga uhusiano kati ya Rais na Naibu wake.

Pia aliomba kanisa kuandaa ibada na maombi maalum kwa Rais Kenyatta na Dkt Ruto ili warejelee uhusiano wao kama zamani jinsi ilivyokuwa kabla ya ujio wa Bw Odinga kupitia salamu za handisheki.

Bi Jumwa naye alipinga mchakato ambao ripoti ya BBI inafaa kupitishwa kabla ya kuishia marekebisho ya katiba na pia kubuniwa kwa kamati ya wataalamu kuangazia mapendekezo yaliyomo ndani yake.

Matamshi ya wanasiasa hao yanajiri baada ya Rais Kenyatta kuwakaripia wandani wa Dkt Ruto wanaopinga mapendekezo ya BBI.

You can share this post!

Sababu ya Uhuru kumfuata Ruto kanisani

Uokoaji waendelea kunusuru waliokwama jengoni Tassia

adminleo