Habari Mseto

Waombwa wahamie nyanda za juu kukwepa mauti

April 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na OSCAR KAKAI

Wakazi wanaoishi katika maeneo hatari ya nyanda za chini katika Kaunti ya Pokot Magharibi wameshauriwa kuhama kutoka maeneo hatari ili kuzuia maafa ya maporomoko ya ardhi yanayoletwa na mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika eneo hilo.

Hii ni baada ya watu 14 kufariki, wengine kupotea na huku wengine wakijeruhiwa vibaya pamoja na mali kuharibiwa kwenye mkasa wa maporomoko ya tope uliotokea katika kijiji cha Chesegon, eneobunge la Sigor baada ya mvua kubwa kunyesha usiku wa Jumamosi.

Maeneo mengi kama vile Sondany, Tapach, Batei, Kerelwa, Muino na Seker ni ya vitakoni mwa miinuko na milima ambapo ni hatari huku tukio la hivi maajuzi likiwa la Chesegon ambapo watu wa kijiji hicho walipoteza makao na mali kuharibika kufuatia mvua kubwa inayonyesha eneo hilo.

Kuumekuwa na ripoti nyingi za maporomoko huku wakazi wakiombwa kuondoka katika maeneo hayo.

Barabara za eneo la Muino hazipitiki baada ya kuvurugwa na mvua kubwa inayonyesha.

Akiongea katika eneo la Chesegon, Mbunge wa Sigor, Bw Peter Lochakapong aliwataka wakazi kuondoka mara moja katika nyanda za chini na kuhamia maeneo salama ili kuzuia maafa ambayo yanaweza kusababishwa na mvua hiyo.

“Tunawapa onyo wakazi sababu eneo hilo huathirika na maporomoko. Maporomoko husababisha uharibifu wa mali na makao ya wakazi kupotea,” alisema.

Bw Lochakapong alisema kuwa asilimia arobaini ya eneo hilo ni milima huku akiwataka wakazi kupanda miti kama njia ya kuzuia mmomonyoko wa udongo.

“Suluhu pekee ambayo imebaki ni upanzi wa miti ili tujiepusha na majanga.”

Alitoa wito kwa wakazi wa eneo hilo kuhama wakati huu akisema kuwa dalili zinaonyesha kuwa mvua hiyo itaendelea kunyesha na kusababisha mafuriko na maporomoko zaidi.

“Wakazi wanafaa kuwa chonjo. Ni vyema watu wanaoishi katika maeneo kama hayo kuchukua tahadhari kabla ya hatari. Watu wasione ugumu kuhama na tunaomba wadau kutusaidia wale ambao tayari wameathirika,” alisema Bw Lochakapong.

Alitoa wito kwa wakazi wa eneo hilo kutojenga nyumba karibu na milima.

Bw Lochakapong aliyezuru waathiriwa katika hospitali ya Kaunti, Kapenguria alisema wakazi wameathirika na mvua kubwa na kutaka shirika la msalaba mwekundu kusaidia jamii hizo.

“Nyumba zingine zimefunikwa na tope na mifugo kubebwa. Ni hasara kubwa sana .Wakazi wanahitaji msaada,” alisema.

Bw Lochakapong alizitaka serikali za kaunti na kitaifa kutuma waatalamu kufanyia uchunguzi eneo hilo na kuwashauri wakazi ambao kuishi kabla ya hali hiyo kuwa mbaya.

“Tunataka hatu kuchukuliwa na idara husika ili kuokoa wakazi,” alisema.

Aliitaka serikali ya kaunti ya Pokot kuuimarisha huduma kwa kuharakisha ufunguzi wa chumba cha wagonjwa mahututi katika hospitali ya kaunti ya Kapenguria ambayo alisema kwa sasa haina huduma za kushughulikia wagonjwa mahututi na wenye wanafaa kupimwa hali ya kichwa .

“Hakuna huduma kupima wagonjwa .Tumelazika kupeleka wagonjwa Eldoret na huku tunaambiwa wamejaa .Tumewapeleka Med heal penye analipa shilingi elfu hamsini kufanyiwa uchunguzi wa kichwa na hiyo ni gharama kubwa,” alisema.